Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TUENDELEE KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA UGONJWA WA MPOX

Posted on: March 15th, 2025

Na WAF - Songea, Ruvuma

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amewataka Watanzania kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Mpox kwa kuepuka kukumbatiana, kushikana mikono, kwakuwa ugonjwa huu unatokana na maambukizi kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na binadamu ana uwezo wa kumuambukiza mwenzake kupitia majimaji.

Waziri Mhagama amesema hayo leo Machi 15, 2025 kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa kinachoongozwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed ambacho kinahudhuriwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Wabunge na Wakuu wa Ulinzi na Usalama.

“Tarehe 7 Machi 2025 tulipata taarifa ya uwepo wa tetesi za wahisiwa wenye dalili za vipele na mambo yanayoendana na ugonjwa wa Mpox, ilipofika tarehe 9 Machi 2025 baada ya kukamilisha uchunguzi wa kimaabara tulithibitisha na kutoa taarifa kuwepo kwa wagonjwa wawili wa ugonjwa wa Mpox,” amesema Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kufatilia kwa kina mwenendo wa ugonjwa huu kwa wale waliotengamana na wagonjwa ili kuvunja mnyororo wa ugonjwa huo na kuhakikisha Watanzania wanakuwa salama na kuumaliza ugonjwa huo kama ilivyokuwa kwa ugonjwa wa Marburg.

“Magonjwa haya ya mlipuko hayana mipaka, ndiyo maana tunakuwa na mifumo ya mitandao kutoka nchi moja kwenda nyingine ili kuwalinda wananchi wake lakini hasa kutoa elimu kwakuwa na utambuzi wa dalili za magonjwa haya na kuchukua hatua za kitaalam zinazoendelea kusisitizwa na wataalam ili kukata minyororo ya kusambaa kwa magonjwa hayo,” amesema Waziri Mhagama.

Vilevile, Waziri Mhagama amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya juhudi katika mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko na kufanikiwa kuumaliza ugonjwa wa Marburg nchini Tanzania kwa siku 54 baada ya kupita siku 42 bila mgonjwa yeyote wa ugonjwa huo.