Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA KIMATAIFA KUHUSU LISHE

Posted on: September 25th, 2025

Na WAF- New York, Marekani

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, ameongoza ushiriki wa Tanzania katika mkutano wa kujadili mikakati ya kumaliza utapiamlo kwa watoto, ulioandaliwa na Serikali ya Ireland leo Septemba 24, 2025, jijini New York, Marekani.

Mkutano huo umehudhuriwa na wadau wa maendeleo na taasisi za Kimataifa zinazojikita kwenye masuala ya lishe, akiwemo mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO)

Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Magembe amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania kukabiliana na changamoto ya utapiamlo, ikiwemo uongozi thabiti na dhamira ya kisiasa inayoonyeshwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Mkataba wa Lishe ulioingiwa na Wakuu wa Mikoa. Mkataba huo unaongeza uwajibikaji na usimamizi wa utekelezaji wa afua za lishe katika ngazi zote za utawala.

Dkt. Magembe amebainisha kuwa Tanzania imeweka mpango mkakati jumuishi wa afua za lishe, uratibu wa masuala ya lishe kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na uhamasishaji wa afua hizo kupitia Kikundi cha Wabunge kinachoshughulikia lishe.

Kwa upande wao, wadau wa maendeleo wamepongeza jitihada zinazofanywa na Tanzania na kuahidi kuendelea kushirikiana na nchi mbalimbali katika kuimarisha afua za lishe, ili kufanikisha lengo la kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa tatizo la utapiamlo miongoni mwa watoto.