Ministry of Health

TANZANIA YAJIPANGA KUJITEGEMEA UZALISHAJI WA DAWA, VIFAA TIBA

Posted on: May 8th, 2026

Na Mvuda Jaffer,WAF -Dar-es-Salaam

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuipa sekta ya Afya msukumo wa juu ili kufikia hatua ya kujitegemea katika uzalishaji wa dawa hatua inayoweka msingi imara wa mageuzi makubwa ya kimkakati kuwekeza kwenye sekta hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Dkt. Johanes Lukumay, amesema hayo leo Mei 8, 2026 wakati wa hafla ya Uwekaji Jiwe la Msingi kwa ajili ya uendelezaji wa Kongani ya Viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba Mloganzila jijini Dar-es-salaam.

“Dira ya maendeleo ya Taifa ya miaka mitano inalenga kuhakikisha Tanzania inajenga uwezo wa kujitegemea katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba ifikapo mwaka 2030, sambamba na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi,” amesema Dkt. Lukumay

Aidha, Dkt. Lukumay amesema mafanikio hayo yatakwenda sambamba na kuongeza ajira kwa vijana, kukuza uchumi wa viwanda na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni yanayotumika katika uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi.

Pia, Dkt. Lukumay amesema ongezeko la ushirikiano kati ya Serikali na wawekezaji wa kimataifa kutoka Marekani, Uingereza, India, Ujerumani na China, akisema hatua hiyo ni ushahidi wa mwamko mkubwa wa uwekezaji katika sekta ya uzalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini.

Mwisho, ameishukuru Serikali na wadau wote kwa ushirikiano wao katika kutekeleza ajenda ya kuifanya Tanzania kuwa nchi inayojitegemea katika sekta ya afya ifikapo mwaka 2030.