Ministry of Health

TANZANIA KUPUNGUZA UTEGEMEZI WA UAGIZAJI BIDHAA ZA AFYA KUTOKA NJE

Posted on: May 8th, 2026



Serikali kupitia Sekta ya Afya inaendeleza dhamira yake ya kupunguza kwa kiwango kikubwa utegemezi wa uagizaji wa dawa na bidhaa za afya kutoka nje ya nchi kwa lengo la kufikia asilimia 85 ya uzalishaji wa ndani ifikapo mwaka 2030.

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema hayo leo Mei 08, 2026 wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la uendeshaji wa kongani ya viwanda vya dawa na vifaa tiba katika eneo la Mloganzira Jijini Dar es Salaam akiambatana na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia Mhe. Angela Kairuki.

"Hatua hii ni mageuzi makubwa yatakayochochea ukuaji wa viwanda vya ndani, kuongeza ajira, kuimarisha teknolojia ya afya pamoja na kuhakikisha Tanzania inakuwa na uwezo wa kujitegemea katika uzalishaji wa dawa na bidhaa muhimu za afya," amesema Waziri Mchengerwa

Aidha, Waziri Mchengerwa amesema lengo la mageuzi ni lengo la kizalendo linalohitaji kasi, uratibu na ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya ujenzi wa viwanda utakaowezesha kuongeza ajira, teknolojia, dawa na chanjo zinakamilika,” amesema Mhe. Mchengerwa

Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa amewapongeza na kuwashukuru wadau na wawekezaji wa bidhaa za afya wote nchini wakiwemo 'Tanzania Pharmaceutical Manufacturers Association' (TPMA) kwa mchango wao mkubwa katika kukuza uzalishaji wa dawa nchini.

Kupitia pongezi hizo, Waziri Mchengerwa amesisitiza umuhimu wa wazalishaji wa bidhaa za afya wa ndani kuendelea kuzingatia viwango vya ubora vya kimataifa ikiwemo GMP ili kuzalisha bidhaa hizo zenye ubora na kumfikia mwananchi.

Pia, Waziri Mchengerwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wa sekta ya viwanda vya dawa na vitendanishi wa ndani na nje ya nchi ambao utaisaidia Tanzania kujenga uwezo wa ndani katika teknolojia ya kisasa ili kukabiliana na changamoto za afya na mahitaji ya soko la kimataifa.

“Hakuna Taifa linaloweza kujenga sekta imara ya dawa bila wazalishaji wake wa ndani kuwa sehemu ya maono, mkakati na utekelezaji kwa kushirikiana na wawekeaji kutoka nje ya nchi,” amesema Waziri Mchengerwa