SERIKALI YATENGA BILIONI ZAIDI YA 80 KWA AJILI YA MATIBABU YA UBINGWA NA UBINGWA BOBEZI.
Posted on: May 13th, 2024
Na WAF, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga kiasi cha shilingi 89,858,609,000 kwa ajili ya kuimarisha huduma za Matibabu ya Ubingwa na Ubingwa Bobezi hapa nchini kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo Bungeni jijini Dodoma mapema leo, Jumatatu Mei 13, 2024 wakati akiwasilisha Hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha wa 2023/24.
Waziri Ummy, amesema Serikali inakusudia kuendelea kutoa huduma za matibabu ya Ubingwa na Ubingwa Bobezi katika Hospitali ya Taifa (Muhimbili), Hospitali Maalum, Kanda na Mikoa pamoja na kuanzisha huduma mpya kulingana na mahitaji yaliyopo.
Ametaja mahitaji hayo kuwa ni pamoja na upandikizaji wa figo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa ya Bungando, upandikizaji wa ujauzito kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma
Ameongeza kuwa Serikali inakusudia kuwekeza kwenye vifaa tiba vitakavyowezesha utoaji wa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi ikiwemo ununuzi wa mtambo wa kupima na kutibu moyo (Cathlab) kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na kuendeleza ujenzi wa miundombinu katika Hospitali sita (6) za Rufaa za Kanda za Chato, Mtwara, Mbeya, KCMC, Bugando, Benjamin Mkapa, ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Magharibi Kigoma na Hospitali 28 za Rufaa za mikoa
Amesema eneo jingine linalotarajiwa kuimarishwa na serikali ni uboreshaji wa utolewaji wa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi na kuendeleza ujenzi wa kituo cha matibabu ya Saratani tawi la Taasisi ya Saratani Ocean Road Mbeya, kuanzisha tawi la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Kanda ya Ziwa (JKCI Chato)
Sambamba na hilo liko suala la kuanza hatua za awali za maandalizi ya Taasisi ya Sayansi ya Tiba ya magonjwa ya Ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu ili kuimarisha huduma za upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu nchini.
Amesema pia kugharamia huduma za matibabu ya ubingwa bobezi ndani ya nchi hususani kupandikiza figo, kupandikiza uloto, kupandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto na kufanya upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu sambamba na kuwajengea na uwezo wataalam wa ndani kutoa huduma hizo kwa umahiri zaidi
Katika hatua nyingine, kwenye eneo hilo Waziri Ummy amesema serikali inakusudia kuanzisha kituo cha umahiri cha upandikizaji uloto na magonjwa ya Damu cha Afrika Mashariki katika Hospitali ya Benjamin Mkapa
Hiyo ikienda sambamba na kuimarisha mifumo ya kielektroniki katika Hospitali zilizoteuliwa ili ziweze kutoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi kupitia Tiba Mtandao (Telemedicine) ndani na nje ya nchi; na kuendelea kutoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi kwa wagonjwa kutoka nje ya nchi (Tiba Utalii)
Mwisho.