SERIKALI YAONGEZA VITUO VYA AFYA KUBORESHA HUDUMA ZA MAMA NA MTOTO
Posted on: September 24th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF – Shinyanga
Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha huduma za afya nchini kwa kuongeza miundombinu, upatikanaji wa vifaa tiba na dawa, juhudi zilizoambatana na kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma za afya kutoka vituo 1,783 mwaka 2023 hadi kufikia vituo 2,424 mwaka 2025 hali inayochangia kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.
Akizungumza leo, Septemba 24, 2026, mkoani Shinyanga wakati akifungua kikao kazi cha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto Kanda ya Ziwa, Kaimu Mwenyekiti wa Kanda hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma na Upasuaji katika Hospitali ya Bugando, Dkt. Samson Kitiba, amesema juhudi hizo zinapaswa kwenda sambamba na mikakati madhubuti ya kuboresha huduma na kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Dkt. Kitiba amesema kikao hicho kina lengo la kutathmini hali ya huduma za afya ya mama na mtoto katika Kanda ya Ziwa, kubaini changamoto zinazochangia vifo vya wajawazito na watoto wachanga, kutafuta suluhisho na kuandaa mipango kazi itakayotekelezwa katika mikoa na halmashauri za kanda hiyo.
“Kikao hiki ni muhimu katika kutathmini hali ya huduma za afya ya mama na mtoto, kubaini changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha huduma hizo, hususan kupunguza vifo vya wajawazito, watoto wachanga na watoto wanaozaliwa wakiwa na uzito mdogo,” amesema Dkt. Kitiba.
Amesema Kanda ya Ziwa ni miongoni mwa kanda kubwa nchini, ikiwa na mikoa sita ambayo ni Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita na Kagera, yenye wakazi takribani milioni 17.8 na halmashauri 43. Kutokana na ukubwa wa kanda hiyo, vikao vya wataalamu vimegawanywa katika makundi mawili ili kuwezesha majadiliano ya kina na kuweka mikakati inayozingatia hali halisi ya kila eneo.
Aidha, amesema pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali, bado kuna changamoto zinazohitaji hatua za pamoja, ikiwemo vifo vya watoto wachanga, upungufu wa watumishi, hususan wataalamu wa huduma za usingizi. Amewataka Waganga Wakuu wa Wilaya na Wafawidhi kutumia fursa ya kikao hicho kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuandaa mikakati ya pamoja inayotekelezeka katika kukabiliana na changamoto hizo.