Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI, WAENDESHA BODABODA WAWEKA MIKAKATI KUTOKOMEZA AJALI

Posted on: May 11th, 2024



Na WAF, DODOMA 


Serikali kupitia Wizara ya Afya imewapa jukumu wadau wa usafirishaji wakiwepo madereva Bodaboda na Madereva wa Mabasi kuwa vinara wa kudhibiti ajali za Barabarani ili kuokoa nguvu kazi ya Taifa. 


Akizungumza katika semina na wadau wa usafirishaji Mei 11, 2024 jijini Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt John Jingu amesema, ajali za Barabarani zimekuwa zikichukua nguvu kazi ya taifa kwa watu walio na umri wa kati ya miaka 19 na 59.


"Mtu mmoja akipata ajali ya barabarani ambaye ndiye mzalishaji, athari zake haziishii kwa mtu binafsi bali pia jamii yake lakini pia Serikali kutumia fedha nyingi ambazo zingeweza kuelekezwa maeneo mengine kwa mustakabali na ustawi wa nchi" amesema Dkt. Jingu.


Dkt. Jingu ameongeza kuwa watu milioni 1.19 wameripotiwa kufariki Dunia kutokana na ajali za barabarani ambazo zinaongoza kwakuuwa watoto na vijana wa miaka 5 hadi 29 huku wanaofariki zaidi wakiwa ni Watembea kwa miguu, waendesha baiskeli na Bodaboda


Aidha Dkt. Jingu amesema kwa mwaka 2023 jumla ya majeruhi 163,148 walipokelewa katika vituo vyakutolea huduma za afya nchini huku mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza, Dodoma na Kagera akiitaja kama mikoa inayo ongoza.


"Jumla ya majeruhi 11,434 walihudumiwa kwenye Hospitali 16 za Rufaa za Mikoa 16 nchini kwa kipindi cha mwezi Juni 2023 hadi Machi 2024 majeruhi wa Bodaboda wakiwa asilimia 61 ya majeruhi wote” amefafanua Dkt. Jingu.


Awali, Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu, akimkaribisha Katibu Mkuu kufungua semina hiyo, amesema shabaha yakuwaita wadau wa usafiri nikuweka Mikakati ya pamoja kukabiliana na ajali Barabarani.


Akitoa mada kwenye Semina hiyo, Kamishna Msaidizi Polisi Mkuu wa Dawati la Elimu kwa umma Makao Makuu, Michael Deleli, ameendelea kuwahimiza wapanda pikipiki kuvaa kofia Ngumu.


"Kichwa hakina mbadala wake, kikiumia huwezi kusema utaweza kubadilisha, rai yangu hakikisha wewe dereva na abiria wako mnajihami kwakuvaa Kofia Ngumu kujikinga na Ajali lakini pia kuacha ulevi wakati wa kazi" amesema ACP Michael Deleli


MWISHO