Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI KUIMARISHA TIBA ASILI NA TIBA MBADALA KWA BIL 1.5

Posted on: May 13th, 2024



Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema serikali imeweka mpango wa kuendeleza na kusimamia afua za Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini, ambapo serikali imetenga kiasi kikubwa cha fedha kwa utekelezaji wake.

Akizungumza wakati wa uwasilishwaji wa Bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2024/25, Waziri wa Afya Mhe. Ummy amefafanua kuwa jumla ya Shilingi 1,500,000,000.00 zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha hatua kadhaa muhimu katika kuboresha sekta hii muhimu ya afya.

Waziri Ummy amesema moja ya hatua kuu ni kuanzishwa kwa Mpango wa Taifa wa Tiba Asili na Tiba Mbadala, ambao unalenga kuweka mifumo madhubuti ya utekelezaji na usimamizi wa tiba hizi mbadala.

Aidha, serikali imeamua kuendeleza huduma za Tiba Asili, ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa mashamba ya miti dawa katika mikoa mbalimbali kwani kupitia hatua hii, wananchi wataweza kupata upatikanaji rahisi wa mimea na vifaa vinavyohitajika kwa tiba mbadala.

Katika kuimarisha miundombinu, Waziri Ummy amesema mpango wa kununua ardhi na kufanya usanifu wa ujenzi wa Hospitali maalum ya kitaifa ya kutoa huduma jumuishi za Tiba Asili na Tiba Mbadala hii ikiwa ni kitovu cha utoaji wa huduma bora na za kisasa za tiba mbadala kwa wananchi.

Pia, serikali imepanga kuongeza idadi ya Hospitali zinazotoa huduma jumuishi za Tiba Asili kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa saba hadi kumi na nne, lengo likiwa ni kufikia idadi kubwa zaidi ya wananchi.

Hatua hizi ni sehemu ya mkakati wa serikali katika kuhakikisha kuwa huduma za afya za Tiba Asili na Tiba Mbadala zinapatikana kwa urahisi na kwa viwango vya juu vya ubora kwa wananchi wote kwakuwa mpango huu unalenga pia kukuza utamaduni wa matumizi ya tiba mbadala kwa kuzingatia utafiti na uhakiki wa kisayansi.