Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI IMETENGA BILIONI 11 KUENDELEZA HOSPITALI YA RUFAA MKOA WA MARA

Posted on: March 26th, 2024



Na WAF - Musoma, Mara

Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga kiasi cha fedha shilingi Bilioni 11 kwa mwaka wa fedha 2023/24 ili kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Kwangwa, iliyopo mkoani Mara.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Machi 26, 2024 akiwa katika ziara yake ya kutembelea Hospitali hiyo kwa lengo la kukagua hali ya ujenzi ilipofikia wakati wa kuelekea kwenye bajeti ya mwaka 2024/25.

“Serikali yetu chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaipa kipaumbele cha juu Hospitali hii ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Kwangwa, Mara ili ukamilishaji ujenzi wake na ndio maana nimekuja kuona hali ilivyo na ilipofikia wakati tukielekea mwisho wa mwaka wa bajeti 2023/24.” Amesema waziri Mhe. Ummy

Aidha, Waziri Ummy amesema Serikali kupitia jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inataka kuimarisha huduma za watoto wachanga wenye umri kuanzia siku 0 hadi 28 kwa kujenga wodi ya watoto wachanga itakayokua na sehemu kubwa tatu katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara.

“Tunataka watoto wachanga wawe na wodi yao maalum, kwa hiyo kutakua na wodi ya watoto waliozaliwa kati ya leo hadi siku 28 ambao watakua na vifaa tiba vyao, lakini na wodi ya watoto waliozaliwa na uzito pungufu (Kangaruu Mother Care) pamoja na wodi ya watoto wachanga mahututi.” Amesema Waziri Ummy

Waziri Ummy amesema, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan tayari ametoa fedha kiasi cha Bilioni 2.5 ili kujenga wodi hiyo katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mtanda ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kutoa Fedha kiasi cha Tsh: Bilioni Nne kwa ajili ya kutatua changamoto ya umeme kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Kwangwa, Mara.

“Tulikua tunasumbuliwa sana na swala la kukatikakatika kwa umeme, tunakushukuru sana Mhe. Waziri kwa kutoa fedha kiasi cha Bilioni Nne ili kutatua changamoto hii, kwa sasa tatizo hili litakua limekwisha katika Hospitali yetu.” Amesema Mhe. Mtanda