Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MTOTO WA MWAKA MMOJA ATOLEWA SHILINGI 100 NA MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA

Posted on: May 16th, 2024

Na WAF, SIMANJIRO MANYARA

Madaktari Bingwa na Bobezi walioweka kambi katika Hospitali ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wamefanikiwa kumtolea shilingi mia mtoto Hidary Abdallah mwenye umri wa mwaka mmoja.

Daktari Bingwa wa Usingizi na Ganzi Benedicto Mwampashi kutoka Muhimbili, amesema mtoto huyo alifikishwa hospitalini hapo siku mbili baada ya kumeza shilingi 100.

"Tulimpokea mtoto Hidary Abdalah akiwa na wazazi wake, wakitokea kijiji cha Ngage wilayani hapa takribani kilometa 57 kutoka hospitali ya wilaya ya simanjiro akiwa anatokwa na mate mengi mdomoni na wazazi wakieleza alikuwa akipata changamoto kula na mara kadhaa shida kupumua. Ilikuwa kama bahati kwani ndio tulikuwa tumefika kwenye kambi hii ya Madaktari Bingwa wa Samia" amesema Mwampasi na kuongeza

"Zoezi la kumuondolea shilingi 100 aliyomeza lilitumia takribani dakika 45 baada ya mtoto kupewa dawa za usingizi na baada ya hapo afya yake iliendelea kuimarika mpaka tulipomruhusu kurejea nyumbani.

Mwampasi amesema isingelikuwa kambi ya madaktari bingwa wa Samia basi mtoto huyu angelazimika kupewa rufaa kwenda mkoani Kilimanjaro (KCMC) au mkoani Arusha (Mount Meru) kwa matibabu.

Kwa upande wao wazazi wa mtoto Abdalah wameishukuru wataalam hao na kusema huduma hiyo ya mkoba imekuwa na faida kwao.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Simanjiro Dkt Abdlin Mtitu, amesema ingekuwa sio huduma ya Madaktari Bingwa, mtoto huyo na wazazi wake wangepatiwa rufani ya dharura kwenda Kilimanjaro au Arusha

MWISHO