Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MKATOE HUDUMA NA ELIMU MLIYOIPATA YA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA - Dkt. SHEKALAGHE

Posted on: June 22nd, 2023

Na. WAF - Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk Seif Shekalage amewataka watoa huduma za afya nchini kwenda kutoa huduma na elimu ya magonjwa yasiyoambukiza kuanzia ngazi ya msingi ili jamii iweze kujitambua na kuchukua tahadhari juu ya magonjwa hayo.

Dkt. Shekalage ametoa wito huo leo wakati akifunga mafunzo ya wataalamu wa afya ngazi ya msingi kutoka kwenye vituo vya afya vya mikoa ya Tanga, Manyara, Tabora na Shinyanga yaliyodumu kwa siku Tano Jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa suala la magonjwa yasiyoambukiza ni tatizo kubwa katika jamii, hivyo Serikali kupitia wizara ya Afya itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kudhibiti magonjwa haya, ikiwemo kutoa Elimu pamoja na Tiba kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Aidha, Dkt. Shekalaghe amesema kuwa Tukiwatumia vizuri viongozi wa ngazi ya chini kama mabalozi, wenyeviti wa vijiji na vitongoji kwa kuwapa Elimu, watasaidia kuwa chachu kubwa ya kufikisha Elimu hiyo kwa wananchi katika ngazi zao.

“Zinahitajika jitihada za pamoja kuhakikisha tunapunguza tatizo hili kwa kutoa elimu kuanzia ngazi ya msingi kwa mabalozi, watendaji na kwenye mikutano ya vijiji ili ujumbe uweze kufika kwa urahisi katika jamii na kuwa na uelewa”. Amesema Dkt. Shekalaghe

Wakati akifunga mafunzo hayo Dkt. Shekalaghe ametoe rai kwa wataalam hao wa ngazi ya msingi wakirudi kwenye vituo vyao kwenda kutoa elimu kwa umma kwa kuwaelimisha wajue magonjwa haya yanasababishwa na nini ili katika familia kama kuna mtu mmoja asiongezeke mwingine.

Pia, Amesema jukumu la kudhibiti ongezeko la magonjwa haya lipo moja kwa moja kwa mtu mwenyewe kuchukua hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na kuishi mtindo bora wa maisha unaofaa, ikiwemo kufanya mazoezi na kuzingatia ulaji bora wa vyakula.

“Lakini pia nitoe rai kwa Watanzania ambao ni lazima wafahamu magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa Saratani, Kansa, Pesha pamoja na Kisukari, ili kuondokana na magonjwa haya jukumu kubwa lipo kwa wananchi wenyewe lazima wazingatie mtindo bora wa maisha”. Amesema Dkt. Shekalaghe