Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MILIONI 140 ZATUMIKA KUKAMILISHA JENGO LA WAHISIWA WA MAGONJWA YA MLIPUKO

Posted on: November 9th, 2024

Na WAF - Dodoma

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa jengo la kuwahifadhi wahisiwa wa magonjwa ya kuambukiza lililopo mpaka wa Mutukula Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera imekamilika.

Dkt. Mollel amesema hayo Novemba 08,2024 Bungeni jijini Dodoma, wakati ajibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Bernadetha Mushashu aliyetaka kujua ni lini jengo la hospitali hiyo litakamilika.

Amesema Serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa jengo la kuwahifadhi wahisiwa wa magonjwa ya kuambukiza lililopo katika mpaka wa Mutukula wilaya ya Missenyi mkoa wa Kagera, ambalo limegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 140. Kwa sasa jengo hilo limekamilika na limewekewa huduma za maji, umeme na vitanda na tayari limeanza kutumika kuwahifadhi wahisiwa wa magonjwa ya kuambukiza,” amesema Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/25 Serikali imetenga kiasi cha fedha kwa ajili ya ukarabati wa nje wa jengo ili kuimarisha utoaji wa huduma katika jengo hilo.

“Katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2024/25 Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Milioni 80 kwa ajili ya maboresho ya sehemu ya nje ya jengo, ikiwemo kuweka sehemu yenye kivuli kwa ajili ya wasafiri pamoja na uwekaji wa viyoyozi na samani nyingine kwa ajili ya utoaji wa huduma,” amesema Dkt. Mollel.

Aidha, Naibu Waziri huyo akijibu swali la nyongeza kuhusu mpango wa Serikali wa kujenga hospitali kubwa ya magonjwa ya mlipuko amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha magonjwa ya mlipuko hayaingii nchini kwa kuweka miundombinu bora na kujikinga katika maeneo yote ya mipakani.