Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MATUMIZI HOLELA YA DAWA, SHINIKIZO LA DAMU NA KISUKARI VYATAJWA CHANZO ONGEZEKO LA MAGONJWA YA FIGO

Posted on: November 5th, 2024

Na WAF - Dodoma

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema matumizi holela ya dawa, hasa za maumivu na zinazotibu magonjwa mbalimbali ya muda mrefu zimetajwa kuwa ni moja ya vichocheo vikuu vya ongezeko la magonjwa ya figo nchini.

Akizungumza bungeni Jijini Dodoma leo Novemba 05, 2024, Dkt. Mollel ameeleza kuwa ongezeko hili linachangiwa zaidi na mambo kadhaa ikiwemo magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu na kisukari pamoja na WAVIU wasiokuwa na ufuasi mzuri wa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI(WAVIU).

Dkt. Mollel amesema kutozingatia mtindo sahihi wa maisha, kama matumizi makubwa ya chumvi, ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi, na matumizi ya vilevi kama pombe na tumbaku, ni sababu nyingine zinazochangia kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wa figo.

Aidha, Dkt. Mollel amesema kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha Bima ya Afya kwa Wote inakua suluhu ya gharama kubwa za matibabu na kwamba mchakato wa kuwashirikisha wadau umeanza ili kufikia malengo ya Bima ya Afya kwa Wote.

"Katika juhudi za kupunguza tatizo hili, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kubadili mtindo wa maisha. Elimu hiyo inahusisha kupunguza ulaji wa chumvi na vyakula vilivyokobolewa, pamoja na kuimarisha huduma za matibabu kwa magonjwa yasiyoambukiza na VVU/UKIMWI ili kuzuia madhara zaidi," amesema Dkt. Mollel.