Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MADAKTARI BINGWA WAFIKA HALMASHAURI SITA MKOA WA LINDI

Posted on: May 28th, 2024



Na WAF -Lindi

Mkoa wa Lindi umekuwa mmoja wa mikoa iliyopokea Madaktari Bingwa 35 kwenye Halmashauri zake sita ikiwa ni muendelezo wa kambi hizo kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Akiwa amemuwakilisha Mkuu wa mkoa huo, Katibu Tawala wa mkoa Bi Zuena Omary Wananchi wa mkoa wa Lindi wamepata fursa ya huduma za kibingwa katika hospitali za halmashauri sita za mkoa kwa siku tano.

Amesema huduma hizo za kibingwa zitahusisha madaktari na wataalamu wa afya kutoka hospitali kubwa na taasisi za kitaifa za afya, ambao watatoa matibabu na ushauri wa kitaalam kwa magonjwa mbalimbali.

"Wananchi wanatarajiwa kupata huduma kama vile upasuaji, huduma za magonjwa ya ndani, afya ya wanawake, huduma za watoto, na huduma za magonjwa ya ndani miongoni mwa zingine" amesema Zuena.

Hatua hii ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali kuboresha huduma za afya vijijini na kuhakikisha kuwa huduma za kibingwa hazipatikani tu mijini, bali pia maeneo ya pembezoni kama Lindi. Wananchi wanashauriwa kutumia kikamilifu fursa hii ili kuboresha afya zao na za familia zao".

Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Lindi ndugu Patrick Seleman uzinduzi wa huduma hizo, ni sehemu ya juhudi za serikali ya CCM kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za afya bila kujali wanapoishi.

Ametoa wito kwa wananchi wa Lindi kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hii muhimu ili kupima afya zao na kupata matibabu yanayostahili.

Mpango huu unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na TAMISEMI, Chini ya mpango wa Madaktari Bingwa Dkt Samia. Lengo kuu ni kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa yanayoweza kutibika na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma bora za afya bila kujali mahali anapoishi.

MWISHO