Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WATAJWA CHACHU KUPUNGUZA MATATIZO YA AFYA TANGA

Posted on: October 21st, 2024

Na. WAF – Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian amesema ujio wa Madaktari Bingwa wa Rais Samia utapunguza matatizo ya afya kwa wananchi wa mkoa huo na mikoa jirani sambamba na kusaidia kutoa mafunzo elekezi kazini kwa watumishi wa sekta ya afya katika hospitali wanapokwenda kutoa huduma.

Ameyasema hayo leo Oktoba 21, 2024 wakati akipokea Madaktari Bingwa wa Rais Samia 77 wanaotarajia kutoa huduma za kibingwa kwa siku sita katika hospitali za halmashauri 11 za wilaya za mkoa wa Tanga mapokezi yaliyoenda sambamba na zoezi la kukabidhi magari 8 kwa Wakuu wa Wilaya yatayotumika na Hospitali za wilaya

Dkt. Burian amewataka madaktari bingwa watakapofika katika hospitali hizo kusaidia kuboresha huduma katika wodi za watoto wachanga (njiti) kwa kufunga mashine za kuhudumia watoto hao katika hospitali ambazo hazijaanza kutoa huduma hizo.

“Nitafurahi mkirudi kutoka katika vituo vyenu mtupe mrejesho ili kujua wapi pa kufanyia kazi ili kuendelea kuimarisha zaidi huduma za afya katika mkoa wa Tanga hata mnapokuja kwa mara nyingine tuwe tumerahisisha kazi yenu,” amesema Dkt. Burian.

Aidha, Dkt. Burian ameishukuru Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kubuni jambo hili lenye lengo la kumfikia kila mtanzania mwenye uhitaji wa matibabu ya kibingwa karibu na maeneo yao na kushukuru madaktari bingwa hao kwa kujitoa kwao kuwahudumia Watanzania.

“Kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Tanga tunawashukuru sana kwa kazi nzuri iliyotukuka, kwa awamu iliyopita zaidi wa wagonjwa 8,000 wamehudumiwa na madaktari bingwa kwani msingekuja wangepata tabu ya kwenda katika hospitali ya Taifa Muhimbili au KCMC Arusha, mmepunguza sio tu gharama lakini kuwaokolea muda wao na kuwafikishia huduma hizo karibu na maeneo yao

Kwa upande wake Mratibu wa Madaktari Bingwa kutoka Wizara ya Afya Bw. Joachim Masunga amesema maelekezo ya Serikali kupita Wizara ya Afya ni kuwajengea uwezo wataalamu waliopo katika hospitali za wilaya ili kupata ujuzi na kuendelea kuwahudumia Watanzania mara baada ya madaktari bingwa kuondoka.