Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MADAKTARI BINGWA WA DKT. SAMIA WAWAJENGEA UWEZO WATAALAM WA KINYWA NA MENO NANYAMBA

Posted on: September 17th, 2025

Na WAF, Mtwara

Wataalam wa kinywa na meno katika Hospitali ya Wilaya ya Nanyamba wamejengewa uwezo wa kutumia teknolojia ya kisasa ya mashine ya digital X-ray kwa ajili ya uchunguzi wa kinywa na meno kupitia kambi maalum ya madaktari bingwa wa Dkt. Samia.

Akizungumza Septemba 16, 2025 , Tabibu wa kinywa na Meno wa Hospitali hiyo Bi. Agnes Filidi ameshukuru ujio wa madaktari hao na kutoa elimu ambayo kwao ni fursa ya kujifunza vitu vingi na kujengewa uwezo wa namna ya kutumia vifaa mbalimbali tulivyonavyo, kutoa huduma za kibingwa na bobezi kwa wananchi wanaotuzunguka.

"Tumefundishwa namna ya kutumia Digital Xray ya meno kufanya uchunguzi, mafunzo hayo tumeanza jana na tutaendelea nayo ili kuwapatia wagonjwa matibabu stahiki," amesema Bi. Filidi.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kinywa na Meno kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Luciana Albert amesema uwepo wa kambi hiyo ni fursa nzuri kwani inatoa nafasi ya kuwafikia wataalam vituoni na kubadilishana ujuzi juu ya mabadiliko ya kisasa yanayotokea katika taaluma.

"Kwangu mimi kama Mtaalam na mwalimu naona ni fursa nzuri ya kuangalia mazao tunayotoka katika vyuo vyetu ili kuishauri Wizara namna gani ya kuboresha kwa sababu tunaona vile wanavyotenda wakiwa kazini," amesema Dkt. Luciana.

Kwa upande wake mkazi wa wilaya ya Nanyamba mkoani mtwara Bi. Elizabeth Njelekela amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ujio wa madaktari hao.

"Nilipo sikia ujio wa madaktari hawa nilifurahi kwani ilinibidi niende hospitali za rufaa za mbali kama muhimbili ili kumpeleka mwanangu aweze kushughulikiwa tatizo lake naamini ujio wa madaktari hawa mwanangu atapona," amesema Bi. Njelekela.