Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MADAKTARI BINGWA 48 KIGOMA NGAO DHIDI YA CHANGAMOTO ZA KIAFYA ZA MPAKANI

Posted on: September 30th, 2025

Na WAF, Kigoma

Madaktari Bingwa 48 kutoka Mpango wa Madaktari Bingwa wa Mama Samia wamewasili mkoani Kigoma kwa ajili ya kutoa huduma za afya za kibingwa kwa wananchi pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa sekta ya afya katika ngazi ya halmashauri.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, CPA Hassan Abbas Rugwa, amewapokea madaktari hao na kusema kuwa ujio wao ni hatua muhimu kwa mkoa huo katika kuimarisha afya ya umma, hasa katika mikoa wa mipakani ambao unahitaji kuwa na mifumo imara ya kinga na tiba.

“Kwa mkoa wa Kigoma, ambao unapakana na mataifa jirani tunakabiliwa na changamoto nyingi za kiafya kutokana na mwingiliano wa watu katika mipaka yetu. Huduma hizi za kibingwa zitatusaidia sio tu kutoa tiba kwa wananchi, bali pia kujenga kinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza kutoka mataifa jirani,” amesema Bw. Rugwa.

CPA Rugwa ameongeza kuwa pamoja na kutoa huduma, wataalam hao pia wataendesha mafunzo kwa watumishi wa afya wa mkoa ili kuwajengea uwezo wa kitaalam, hatua itakayosaidia kuimarisha huduma hata baada ya kampeni hiyo kuisha.

“Uwepo wa madaktari hawa si kwa ajili ya kutoa huduma pekee, bali pia kuimarisha mifumo yetu ya afya kupitia mafunzo kwa watumishi wetu wa ndani. Hii ni fursa muhimu kwa ustawi wa huduma za afya Kigoma,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mratibu wa Madaktari Bingwa Mkoa wa Kigoma, Bi Grace Mariki amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya za kibingwa na bingwa bobezi, huku pia ikijenga msingi wa uendelevu kupitia mafunzo kwa watumishi wa afya waliopo.

“Lengo letu ni kuleta huduma karibu na wananchi, hasa wale walioko maeneo ya pembezoni ambapo mara nyingi wamekuwa wakikosa huduma hizi muhimu. Lakini pia tunahakikisha tunawaachia wataalam wetu ujuzi wa kuendeleza huduma hizi kwa muda mrefu,” amesema Bi. Mariki.

Madaktari bingwa hao ni pamoja na bingwa wa usingizi na ganzi salama, bingwa wa watoto, bingwa wa magonjwa ya ndani, bingwa wa upasuaji na bingwa wa wanawake.