Ministry of Health

KONGANI YA MLOGANZILA KUPUNGUZA GHARAMA ZA UWEKEZAJI

Posted on: May 8th, 2026

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Kongani ya Viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba ya Mloganzila inalenga kujenga mfumo imara wa uzalishaji utakaoipunguzia Tanzania utegemezi wa bidhaa za afya kutoka nje, huku ikiongeza ushindani wa viwanda vya ndani na kuvutia teknolojia za kisasa.

Mhe. Mchengerwa amesema hayo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la maendeleo ya kongani hiyo jijini Dar es Salaam leo Mei 8, 2026 Mhe. Mchengerwa amesema maendeleo ya sekta ya afya hayawezi kutegemea ununuzi wa vifaa pekee, bali yanahitaji uwekezaji katika rasilimali watu wenye uwezo wa kuendesha, kuboresha na kubuni teknolojia hizo.

“Teknolojia ya kweli haihamishwi kwa kununua mashine pekee; huhamishwa kwa kujenga watu wanaoweza kuendesha, kutengeneza, kuboresha na kubuni upya mashine hizo,” alisema Mhe. Mchengerwa.

Mhe.Mchengerwa ameongeza kuwa mfumo huo utawezesha wawekezaji kutumia miundombinu ya pamoja ikiwemo umeme wa uhakika, maji ya viwandani, mifumo ya majitaka, maabara za ubora, maghala pamoja na huduma nyingine muhimu ambazo kwa kawaida huwa na gharama kubwa kwa mwekezaji mmoja mmoja.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema uwepo wa viwanda katika eneo moja utaimarisha minyororo ya ugavi wa malighafi, huduma za kiufundi pamoja na mifumo ya usafirishaji, jambo litakalopunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na la kimataifa.

“Mfumo wa cluster pia utarahisisha udhibiti wa ubora na ufuataji wa viwango vya dawa kwa kuwezesha uwepo wa maabara za pamoja, vituo vya mafunzo na mifumo ya usimamizi wa mazingira inayokidhi mahitaji ya sekta ya afya,” amesistiza Mhe. Mchengerwa.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo alisema Serikali kupitia PIAT imeweka mfumo wa “one-stop governance” utakaorahisisha uratibu wa masuala ya uwekezaji ikiwemo vibali, leseni, miundombinu na tathmini za mazingira, hatua itakayowawezesha wawekezaji kuanza shughuli zao kwa haraka zaidi.

“Wawekezaji wakubwa hawafuati maneno; hufuata mifumo. Mloganzila ni ushahidi kwamba Tanzania imedhamiria kujenga mfumo,” alisema.