Customer Feedback Centre

Ministry of Health

KIFO CHA MARIAM CHANZO NI WAHUDUMU WA AFYA SIO KUKOSA FEDHA

Posted on: November 27th, 2023

Na. WAF - Tanga

Tume iliyoundwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kuchunguza kifo Cha mjamzito, Mariam Zahoro imebaini kuwa kifo hicho kilitokana na uzembe wa wataalam wa Afya na sio sababu ya kukosa fedha za kugharamia matibabu yake kiasi cha Tsh: 150,000.

Waziri Ummy amesema hayo leo Novemba 27,223 baada ya kupokea taarifa kutoka kwa tume ya Uchunguzi aliyoiunda ikiongozwa na Dkt. Ally Said ambae ni Daktari bingwa na Mhandiri wa Magonjwa ya Akina Mama na Uzazi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

“Kifo cha Mariam Zahoro kilitokea tarehe 11 Novemba, 2023 katika kituo cha Afya cha Kabuku baada ya kushindwa kujifungua kwa njia ya kawaida na hivyo kuhitaji kufanyiwa huduma ya dharura ya upasuaji ambapo huduma hiyo hakupatiwa kwa wakati na hivyo kupelekea kupoteza maisha.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, kifo hicho kimetokea kwa sababu ya Mtaalamu wa huduma ya Usingizi na ganzi kutopatikana licha ya kupigiwa simu mara kadhaa kuwa kuna dharura pamoja na Daktari wa zamu namba 2 kuchelewa kufika licha ya kupigiwa simu mara nyingi kuwa kuna dharura.

“Daktari huyo namba 2 xxx hata alipofika hakuchukua hatua za kuokoa maisha ya mgonjwa kama kumpa rufaa baada ya mtaalamu wa usingizi kutopatikana au kutuma mtu wa kwenda kumgongea mtaalam wa huduma za usingizi.” Amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amesema Nchi yetu inaongozwa na Sheria na taratibu hivyo amelitaka Baraza la Madaktari Tanzania pamoja na Baraza la Wauguzi ambao wamepelekewa taarifa za Madaktari hao kuharakisha Mchakato wa Kusikiliza mashauri baada ya kukamilika kwa muda wa siku 14 baada ya wao kujieleza huku akisisitiza watumishi hao kutorudi kazini.

Pia, Waziri Ummy amepiga Marufuku kwa Viongozi na wataalamu kufanya maamuzi ya kuwatoza fedha wananchi kupitia vikao vya makubaliano pasi na kuwashirikisha wananchi kutokana na Majibu ya taarifa ya Uchunguzi kuonyesha kuwa yaliweka makubaliano ya kuwatoza wajawazito gharama hizo za Shilingi laki na nusu kwa watakojifungua kwa Upasuaji.