KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YASISITIZA USIRI WA HUDUMA KWA WATEJA
Posted on: October 12th, 2024
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imesisitiza umuhimu wa kuzingatia usiri katika utoaji wa huduma kwa watu, hasa wenye Virusi vya Ukimwi (VVU), ili kuendelea kutimiza azma ya Serikali ya kuboresha huduma bora za afya kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hassan Mtenga, wakati wa ziara yao katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, Oktoba 11, 2024 ambapo ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa kutoa huduma bora na kwa kuzingatia faragha ya wagonjwa.
Aidha Mhe. Mtenga, ameeleza kuridhishwa kwake na huduma zinazotolewa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, hususan kwenye Kituo cha Tiba na Kitengo kwa watu wenye Virusi vya Ukimwi (CTC) akisema kuwa utunzaji na weledi unaoonyeshwa na watumishi wa hospitali hiyo ni wa kiwango cha juu na unaakisi azma ya Serikali ya kuboresha huduma za afya nchini.
“Huduma bora na usiri ni nyenzo muhimu za kuwafanya wagonjwa kuwa na ujasiri wa kutafuta matibabu na kufuata ushauri wa madaktari bila hofu ya kubaguliwa,” amesema Mhe. Mtenga.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amebainisha kuwa usiri ni jambo la msingi katika kuhakikisha watu wanapata matibabu bila hofu ya unyanyapaa.
Pia, Dkt. Mollel, amesema kuwa Serikali imewekeza kwenye miundombinu, vifaa na vifaa tiba ili kuongeza kasi ya uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi kwani mpaka sasa zaidi ya watu 21,000 kutoka mataifa ya nje wameingia nchini kutibiwa.
"Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza kwenye sekta ya afya ili wananchi wapate huduma bora na kwa hilo tunampongeza na juhudi zake kwani mpaka sasa zaidi ya watu 21,000 kutoka mataifa ya nje wameingia nchini kufuata huduma za afya na hii ni kutokana na ubora wa huduma nchini," amesema Dkt. Mollel
Aidha, Dkt. Mollel, ameishukuru Kamati kwa kuthamini juhudi za Serikali kwa kubainisha kuwa, huduma bora na kuridhishwa kwa wateja ni vipaumbele vya Serikali ili kuimarisha afya za wananchi na kuendeleza jitihada za kukabiliana na UKIMWI na magonjwa mengine.