Customer Feedback Centre

Ministry of Health

JOPO LA MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA YATIA KAMBI MKOA WA MTWARA.

Posted on: May 27th, 2024



Na WAF – Mtwara

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Kenan Sawala amesema wananchi wa mkoa huo wako tayari kupatiwa matibabu bora ya kibingwa kutoka kwa jopo la Madaktari Bingwa wa Rais Samia na kuwaahidi ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa kambi hiyo.

Kanali Sawala Amesema hayo leo Mei 27, 2024 wakati wa uzinduzi na mapokezi ya jopo la Madaktari bingwa wa Rais Samia watakao weka kambi ya siku tano na kutoa huduma za kibingwa kwenye hospitali za Wilaya za mkoa wa Mtwara.

Kanali Sawala amesema ana imani kubwa kuwa madaktari bingwa hao watawafikia watanzania na wafikia lengo la kuwapunguzia changamoto za maradhi na kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara, ili kufanikisha hilo amewahakikishia kuwawekea mazingira rafiki ya kutekeleza utendaji kazi wa madaktari hao.

Pia amemshukuru Rais Samia kwa uanzishwaji wa kampeni hiyo ambayo inakwenda kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Mtwara wanapatiwa huduma za kibingwa karibu na maeneo yao pamoja, na kuboresha miundombinu ya sekta ya afya kwa kujenga hospitali na zahanati za kutosha jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa tiba utalii mkoani huo.

“Huu ni upendo mkubwa unaooneshwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapeleka madaktari bingwa karibu na wananchi ili kutatua changamoto zao, pia Dkt. Samia tunamshukuru kwa maboresho makubwa aliyoyafanya kwenye sekta ya afya jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa kwa ongezeko la tiba utalii, raia wa msumbiji wamekuwa wakija Mtwara kupatiwa matibabu”. Amsema Kanali Sawala.

Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa wilaya ya Mtwara Mjini Mhe. Mwanahamisi Munkunda akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya za Mkoa wa Mtwara amesema wamejipanga vyema kwa kuwapa ushirikiano madaktari bingwa wa Rais Samia na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye hospitali zilizotengwa kwa ajili ya utoaji wa huduma hizo za kibingwa.