Customer Feedback Centre

Ministry of Health

IRINGA WAJIPANGA KUFIKIA ASILIMIA 70 YA WATU WALIOCHANJA IFIKAPO SEPTEMBA 2022

Posted on: August 21st, 2022



Na Englibert Kayombo WAF, Iringa.

Serikali katika Mkoa wa Iringa imejipanga kuongeza hamasa ya uchanjaji na Elimu ya Chanjo dhidi ya UVIKO-19 ili kuwa na idadi ya watu wengi wenye kinga ya Jamii kutoka asilimia 48 ya watu waliochanja hadi kufikia asilimia 70 ifikapo mwishoni mwa Mwezi Septemba mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Halima Omary Dendego kwa wanahabari mara baada ya kutembelea vituo vya utoaji chanjo ya UVIKO-19 kwenye ziara ya Mwakilishi Mkazi wa Shirika la USAID nchini Bi. Kate Somvongisiri kuona hali ya utoaji chanjo Mkoani Iringa.

“Mkoa wetu upo asilimia 48 ya uchanjaji na tunatakiwa kutimiza asilimia 70 ifikapo mwishoni mwa Mwezi Septemba, sisi tutaendelea kuhamasisha na kutoa elimu zaidi ya Chanjo dhidi ya UVIKO-19” amesema Mhe. Dendego.

Mojawapo ya mkakati wa kuhamasisha zaidi Wananchi wengi kupata chanjo ya UVIKO-19, Mhe. Halima amesema kuwa leo Jumamosi ya Agosti 20, 2022 kutakuwa na Tamasha la Muziki litakalohusisha wasanii na watu maarufu ambao wanatumia jukwaa hilo kuhamasisha na kuelimisha zaidi wananchi kujitokeza kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19.

Aidha, Mhe. Dendego ameishukuru USAID, FHI360 pamoja na wadau wengine wanaoshirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya UVIKO-19

Kwa upande wake Bi. Kate Somvongisiri amepongeza jitihada na mikakati iliyopo na inayofanywa na Serikali katika kutoa elimu na hamasa ya Chanjo dhidi ya UVIKO-19.

“Tumezunguka, Sokoni na kwenye kituo cha mabasi, ninapenda kutambua juhudi za wafanyakazi wa huduma za afya, wanafanya kazi nzuri Sana kutoa huduma ya Chanjo kwa wananchi” amesema Bi. Kate Somvongisiri

“Kwa niaba ya watu wa marekani ninajivunia kufanya kazi na Tanzania kufikia malengo ya kitaifa ya kuchanja watu na kulinda maisha ya watanzania” amesema Bi Kate.

Bi. Kate amewashauri wananchi kujitokeza kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19 na kusema kuwa chanjo ni salama na haina madhara yeyote kwa binadamu