Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HUDUMA ZA MADAKTARI BINGWA NI BORA, SALAMA, ZAKUWANUFAISHA WATANZANIA

Posted on: May 16th, 2024


Na WAF, Ikungi-Singida

Mganga Mkuu wa wilaya ya Ikungi Dkt Dorilisa Mlenga amewata wananchi wa wilaya ya Ikungi kujitokeza kwa wingi katika huduma za kibingwa kutoka kwa madaktari bingwa wa Rais Samia na kusema kuwa huduma hizo ni bora, salama na zenye nia njema ya kuweza kuwanufaisha watanzania

Dkt. Dorilisa ameyasema hayo katika kambi ya madaktari Bingwa iliyofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida na kuwatoa hofu wananchi kuhusu huduma hizi muhimu, akisisitiza kuwa zina lengo la kuwanufaisha watanzania wote.

Aidha Dkt. Dorilisa amesema kuwa madaktari hao wameleta ujuzi na mbinu za kibingwa ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora na salama hivyo kupunguza rufaa na gharama za matibabu kwa wananchi

"Dhamira ya serikali ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi, Tunataka kuwapunguzia adha ya gharama kwa kutoa huduma bora na zenye nia njema." Amesema Dkt. Dorilisa.

Pia, Dkt. Dorilisa ameiomba serikali kuendeleza kampeni ya kupeleka madaktari bingwa wa Rais Samia mara kwa mara ili kufikia wananchi wengi zaidi wanaohitaji huduma hizo kwani kupitia kampeni hii wameweza kuwaona wagonjwa hadi 100 kwa siku.

Kampeni hii inalenga kuimarisha huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata matibabu ya hali ya juu karibu na makazi yao, huduma hizi zimeweka matumaini mapya kwa wananchi wa Wilaya ya Ikungi, na zinaashiria azma ya serikali katika kuboresha sekta ya afya nchini.

Mwisho.