Customer Feedback Centre

Ministry of Health

FUATENI MAELEKEZO SAHIHI YA WATAALAMU WA DAWA ILI KUEPUKA USUGU WA VIMELEA DHIDI YA DAWA.

Posted on: September 22nd, 2024

Na WAF- DSM.

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bw. ismail Rumatila ametoa wito kwa wananchi kufuata maelekezo sahihi ya Wataalamu wa dawa ili kuepuka changamoto ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa inayoendelea kukua kwa kasi Tanzania na Duniani kwa ujumla.

Bw. Rumatila amesema hayo leo Septemba 21, 2024 katika matembezi km 5 na km10 yenye ujumbe wa mapambano ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa (UVIDA) yaliyoandaliwa na Wafamasia katika viwanja vya chuo cha Muhimbili Jijini Dar es Salaam.

"Tunajenga mwamko mpya kwenye jamii yetu, tukisisitiza umuhimu wa kufuata maelekezo sahihi ya wataalamu wa dawa, kuepuka matumizi ya dawa kiholela," amesema Bw. Rumatila.

Ameendelea kusema, ni muhimu kufuata ushauri na maelekezo ya Wataalamu wa dawa kwa kuhakikisha kuwa tunamaliza dozi zote tunazopewa na watoa huduma za afya hivyo itasaidia kulinda afya ya mwili.

Sambamba na hilo, amebainisha kuwa, tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa limazidi kuwa tishio Tanzania na Duniani kwa ujumla, huku akieleza kuwa kulingana na WHO inakadiria kuwa ifikapo mwaka 2050, watu milioni 10 watakuwa wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na maambukizi yanayotokana na vimelea sugu.

Kwa upande wake Rais wa chama cha wafamasia Tanzania (PST) Bw. Fadhili Hezekia amesema kuwa, suala la dawa na afya sio biashara, hivyo kutoa wito kwa wafanyabiashara wa dawa kufuata miongozo na taratibu za utoaji huduma za dawa ili kusaidia katika mapambano dhidi ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa.