Customer Feedback Centre

Ministry of Health

DKT. MPANGO ATAKA KIWANDA CHA IDOFI KUANZA KUZALISHA DAWA IFIKAPO JANUARI, 2024

Posted on: October 26th, 2023


Na WAF - Njombe


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameitaka  Wizara ya Afya na Bohari ya Dawa (MSD) kuhakikisha ifikapo Januari 2024 kiwanda cha Dawa Idofi kikichopo Makambako mkoani Njombe upande wa dawa kiwe kimeanza kuzalisha licha ya kuzalisha gloves ili kuendelea kuleta tija kwa wananchi. 


Dkt. Mpango ametoa  agizo hilo leo 26 Oktoba, 2023 Mkoani  Njombe mara baada ya kuweka jiwe la  msingi katika kiwanda cha kutengeneza mipira ya Mikono (Gloves) kinachosimamiwa na Bohari ya Dawa (MSD).


Ameeleza kuwa lengo la kiwanda hicho ni kuhakikisha wanaboresha Huduma kwa jamii na kuimarisha afya za wananchi kwa kuzalisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini.


Dkt. Mpango amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Uongozi imara wa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwezesha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa kuipatia mtaji Bohari ya Dawa ili kujenga viwanda zaidi vya dawa, maghala na kuongeza upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini.


“Serikali inatambua vita iliyopo katika ujenzi wa viwanda vya dawa lakini kwa kuwa uamuzi huo ni wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hakuna atakayefanikiwa kuvikwamisha hivyo vitajengwa kwa manufaa ya taifa.


“Kwa sasa  serikali inaagiza dawa kwa asilmia 80 na vifaa tiba kwa asilimia 90 kutoka nje ya nchi, hali inayosababisha uhaba wa vifaa na gharama kubwa za uagizaji wa vifaa vya afya  hivyo ni lazima kuchukua maamuzi magumu ili kuweza kujitengemea katika upatikanaji wa dawa nchini”. Ameeleza Dkt. Mpango.


Dkt. Mpango amesisitiza kuwa Rais  Samia ameamua viwanda vya dawa vijengwa kwa gharama yeyote kwa kuwa nchi ina uhaba  wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara.


“Tumeamua kuipatia MSD majukumu manne ambayo ni uzalisha, ununuzi, utunzaji na usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini hivyo ni niwahakikishie viwanda hivi vitajengwa nchini kwa maslahi ya taifa letu”, amesema Dkt. Mpango.


Hata hivyo ameongeza kuwa Ujenzi wa viwanda hivyo umelenga kuongeza upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, na vitendanishi ili  kupunguza matumizi ya fedha za kigeni, uhaba wa dawa, gharama kubwa za kuagiza bidhaa hizo nje ya nchi  na kutoa ajira kwa wananchi.



“Uwepo wa kiwanda hiki ni muhimu sana kwa ajili ya mahitaji ya ndani na nje ya nchi wakati wa Corona tulihangaika sana matumizi ya mipira ya mikono (gloves) ni makubwa kiwanda hiki ni mkombozi hivyo lengo la Rais Dk. Samia lazima litimie kwa asilimia 100". Amesisitiza Dkt. Mpango.


Aidha, ameagiza MSD kuongeze uzalishaji mwingine wa maji tiba na vitendanishi na kampuni Tanzu ya MSD zingatieni misingi ya kibiashara na watumishi zingatieni weledi na uzalendo katika kutimiza majukumu yao.


Dkt. Mpango ameelekeza watumishi wote MSD wafanyiwe uchunguzi wale wanaotumiwa na wafanyabiashara kwa maslahi ya mifuko yao wachukuliwe hatua.


“Ukipewa dhamana katika taasisi za umma zingatia maadili, weledi, misingi na miiko ya kazi pamoja na uzalendo”. Ametoa wito Dkt. Mpango.