Customer Feedback Centre

Ministry of Health

DKT. MOLLEL AIPONGEZA SMZ UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA AFYA

Posted on: March 1st, 2025

Na, WAF-Zanzibar

Naibu Waziri wa Afya Tanzania Bara, Dkt. Godwin Mollel ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa uwekezaji wa zaidi ya Shilingi Bilioni 356 katika Sekta ya Afya ambao umeleta mageuzi makubwa ya utoaji wa huduma bora za afya.

Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, akizungumza mara baada ya kushiriki kwenye matembezi maalum ya uzinduzi wa kampeni ya “We Are Equal” yaliyoongozwa na Mama Mariam Mwinyi, Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kushirikisha wake wa Marais kutoka Kenya na Burundi.

“Kupitia uwekezaji wa zaidi ya Bilioni 356, kati ya m waka 2020 hadi 2024tumeona maboresho makubwa katika huduma za afya za msingi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa hospitali zinazotoa huduma za Watoto njiti mahututi kutoka moja hadi 13, vifo vya akina mama wakati wa kujifungua kupungua ni ushahidi wa dhamira yetu ya kulinda maisha ya watoto wachanga na mama ambayo yanayotokana na kuboresha vifaa tiba na kuongeza wataalamu wa afya,” amesema Dkt. Mollel.

Aidha, Dkt. Mollel ameipongeza Zanzibar kwa kuanza kutoa huduma za upasuaji wa nyonga na magoti bandia, ambapo wagonjwa 50 tayari wamenufaika pamoja na huduma za kusafisha figo (dialysis) katika hospitali za Lumumba na Abdalla Mzee, zikirahisisha upatikanaji wa huduma za magonjwa sugu bila hitaji la kusafiri nje ya visiwa hivyo.

Kwa upande wake Mama Mariam Mwinyi, Mke wa Rais wa Zanzibar ambae ni Mwenyekiti wa Bodi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation amesema kuwa Kampeni hiyo imelenga kuwakutanisha wake wa Marais wa Afrika katika kuimarisha huduma za afya nchini.

Wake wa Marais mbalimbali wameshiriki Kampeni hiyo ikiwa ni pamoja na Kenya, Burundi na Angola.

Mafanikio haya ni ishara ya juhudi za serikali ya Zanzibar, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kama China, katika kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya, zenye viwango vya kisasa na vinavyopatikana kwa urahisi