Customer Feedback Centre

Ministry of Health

ALIYETESEKA KWA MIAKA 10 NA MYOMA AFUNGUKA, AWASHUKURU MADAKTARI WA RAIS SAMIA GEITA

Posted on: May 2nd, 2024



Na WAF, GEITA

Bi. Evelina Paul mkaazi wa Biharamulo mkoani Kagera, amewashukuru Madaktari Bingwa na Bobezi walioweka kambi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita baada yakufanikisha kumtolea uvimbe wenye kilo tano uliokuwa umejenga nje ya kizazi ujulikanao kwa jina la Myoma

"Niliteseka na huu uvimbe kwa miaka 10, kulala kwangu, kutembea kulikuwa kwa shida, nilikuwa nasikia maumivu yasiyokoma, nilijaribu kwenda kituo cha afya huko Biharamlo lakini nilipewa dawa zakutuliza Maumivu." amesema Bi Evalina.

Bi. Evelina mama watoto 12, anasema mara baada yakusikia ujio wa kambi ya madaktari Bingwa na Bobezi ilimlazimu kuchukua hatua kusafiri kwenda Geita anapoishi mwanae kwa ajili yakuwaona wataalam hao, ambapo mwanae alimpeleka kwa ajili ya uchunguzi na kugundulika tatizo lake.

Akizungumza mara baada ya kumfanyia upasuaji na kumtolea Uvimbe Daktari Bingwa wa Magonjwa ya wanawake na uzazi Ajee Isack anasema mgonjwa huyo alifika hospitalini hapo Aprili 30, 2024 na kufanyiwa uchunguzi.

"Mara baada ya uchunguzi tulibaini pia alikuwa na shinikizo la juu la damu, hali iliyotulazimu kumtibu kwanza ndio tukamfanyia upasuaji na kuondoa Uvimbe huo wa Myoma ulikuwa na uzito wa Kilo 5.

Dkt. Ajee amesema, chanzo cha Ugonjwa huo huweza kuwapata wanawake wanene, lakini pia watumiaji wa vichocheo vya homoni.

"Chakusahangaza Mgonjwa huyu hakuwa mnene lakini, amepata tatizo hili, nadhani ni wakati sasa wakuongeza tafiti nakujua vyanzo Vingine amesema Dkt. Ajee.

Nao ndugu wa Bi Eveline, wameishukuru Serikali kwa kambi hiyo ya Madaktari Bingwa kusogezwa karibu na wananchi huku wakiomba iwe ni kambi endelevu.

Jopo la Madaktari Bingwa watu, Dkt. Samweli Ndulila, Dkt. Ajee Isack na Dkt. Maufi walifanikisha zoezi hilo.

MWISHO