AFYA YA MSINGI, NGUZO MUHIMU YA MFUMO IMARA NA STAHIMILIVU SEKTA YA AFYA
Posted on: September 11th, 2026Na Andrea Kadege, WAF – Arusha
Wizara ya Afya imesema huduma imara za afya ya msingi ni nguzo muhimu ya kujenga mfumo wa afya unaostahimili changamoto, wenye usawa na endelevu, huku ikisisitiza umuhimu wa kutafsiri maazimio na mapendekezo ya wadau kuwa vitendo vinavyoboresha huduma kwa wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, Mkurugenzi wa Idara ya Dharura na Maafa Dkt. Erasto Sylvanus, amesema mijadala ya siku tatu iliyowakutanisha wataalamu na wadau mbalimbali imezalisha maarifa na suluhisho zinazopaswa kutumika kuimarisha mifumo ya afya nchini na kuchangia kufikia huduma ya afya kwa wote.
"Kuimarisha afya ya msingi hakuhitaji miundombinu pekee, bali kunahitaji watumishi wa afya wenye uwezo na motisha, ufadhili endelevu, upatikanaji wa dawa na teknolojia za kitabibu, mifumo imara ya jamii, huduma bora za kitabibu na mifumo ya kuboresha ubora wa huduma" amesema Dkt. Sylvanus
Amesema wananchi hukutana na mfumo wa afya kwa mara ya kwanza kupitia huduma za afya ya msingi, hivyo ngazi hiyo ni muhimu katika kuzuia magonjwa, kubaini vitisho vya kiafya mapema na kuchukua hatua kwa wakati.
Aidha, amesema kuna umuhimu wa kuimarisha utayari wa kukabiliana na dharura za afya kwa kutumia mifumo ya utabiri na tahadhari za mapema, pamoja na kuimarisha afua za lishe ambazo ni sehemu muhimu ya kuboresha afya ya wananchi.
Ameeleza kuwa Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha mapendekezo na maarifa yaliyoshirikishwa katika mkutano huo yanatekelezwa na kuleta matokeo katika sekta ya afya.