AFYA YA JAMII YAWEKEWA MKAZO KATIKA UTAYARI WA KUKABILIANA NA DHARURA ZA AFYA
Posted on: September 10th, 2026Mkurugenzi wa Idara ya Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Erasto Sylvanus, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha utayari wa kukabiliana na dharura za afya kuanzia ngazi ya jamii na mamlaka za serikali za mitaa, akieleza kuwa hatua za awali za dharura mara nyingi huanzia kwa mtu, familia au jamii kabla ya kufikia ngazi ya kitaifa.
Akizungumza leo Septemba 10, 2026 katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi (IPHCC2026), Dkt. Sylvanus amesema Afrika haina upungufu wa sera, mipango na mikakati ya kukabiliana na dharura za afya, bali changamoto kubwa ipo katika kuhakikisha mipango hiyo inatekelezwa kwa ufanisi, hususan na wahudumu wa afya wa mstari wa mbele, jamii na mamlaka za eneo husika.
“Tunapaswa kuhamisha utayari kutoka ngazi ya Kitaifa na Kikanda kwenda kwenye utayari wa ngazi ya jamii, tukio la dharura huanza kwa mtu mmoja, familia au kijiji kabla halijawa tatizo la nchi nzima,” amesema Dkt. Sylvanus.
Amesema ni muhimu kila Halmashauri kuwa na wasifu wa vihatarishi vya afya (Health Risk Profile) unaoainisha majanga na milipuko inayoweza kutokea katika eneo husika, vipindi ambavyo vihatarishi hivyo vinaweza kujitokeza, pamoja na uwezo uliopo wa kutambua, kutoa taarifa na kuchukua hatua kwa wakati.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa vituo vya kutolea huduma za afya na wahudumu wa afya kuwa sehemu muhimu ya mfumo wa tahadhari ya mapema, huku jamii ikiwezeshwa kutambua viashiria vya hatari, kutoa taarifa kwa wakati na kuchukua hatua stahiki.
Amesisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia nchi kuimarisha uwezo wa kutambua, kutoa taarifa na kukabiliana na dharura mapema, kabla hazijasambaa na kusababisha madhara makubwa katika jamii.