WAKUFUNZI CHUO CHA AFYA PHCI WAFUNDWA KUTOA ELIMU YA KISASA KWA WANAFUNZI WAO
Posted on: July 14th, 2026Na WAF - Iringa
Wakufunzi wa Taasisi ya Afya ya Msingi Iringa (PHCI) wamepewa mafunzo jinsi ya kutoa elimu bora ya afya ya uzazi, mama na mtoto kwa wanafunzi ili kuwapika kuwa wataalamu bora zaidi ili kuendana na mahitaji ya huduma za kisasa kuweza kuokoa vifo vitokanavyo na afya ya uzazi.
Akiongea wakati wa mafunzo hayo Julai 14, 2026, Mratibu wa mafunzo kutoka Wizara ya Afya Bw. Michael Mbele, amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuweka kipaumbele kwa kuwajengea uwezo wataalam wanaotoa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kuhakikisha huduma hizo zinakua bora na salama.
Bw. Mbele amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau imeweka kipaumbele cha kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kuhakikisha huduma za afya zinazotolewa nchini zinakua bora kwa kuzalisha wahitimu wenye maarifa na ujuzi unaoendana na kasi ya mabadiliko ya dunia.
“Ubora wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto huanza na ubora wa mafunzo yanayotolewa kwa wataalamu wa afya, hivyo wakufunzi wana nafasi ya kipekee katika kuzalisha wahitimu wenye maarifa, ujuzi na maadili yatakayowezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi hususan katika eneo nyeti la masuala ya uzazi," amesema Bw. Mbele.
Naye Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Wizara ya Afya Bw. Joachim Masunga ambae ametoa mafunzo ya namna ya kutumia vitabu vya kufuatilia maendeleo ya afya ya uzazi, mama na mtoto, amesema kupitia mafunzo hayo kwa wakufunzi wa vyuo vya kati yamelenga kuwajengea uwezo ambapo wakufunzi hao watatoa elimu hiyo kwa wananfunzi wao namna ya kutumia vitabu hivyo ili kutoa huduma bora za uzazi kwa wananchi.
Mafunzo hayo kwa wakufunzi wa vyuo vya kati yanafanyika katika mikoa mbalimbali nchini ambapo kwa mikoa ya nyanda za juu kusini yatatolewa katika vyuo vya kati vya mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe.