Wizara Ya Afya

SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA MAFUNZO YA KADA ZA AFYA KWA LENGO LA KUINUA UBORA WA HUDUMA

Posted on: September 27th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Dodoma

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuboresha mafunzo na maendeleo ya kada za afya nchini ili kuhakikisha wahitimu wanaozalishwa wanakuwa na maarifa, ujuzi na uwezo unaokidhi mahitaji ya sasa ya utoaji wa huduma bora za afya.

Mhe. Mchengerwa amesema hayo leo Agosti 27,2026 wakati akiwasilisha taarifa ya Serikali kuhusu utekelezaji wa maoni na ushauri uliotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kwa kushirikiana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, katika kikao kilichojikita katika masuala ya sekta mtambuka kati ya Afya na Elimu.

Amesema Serikali, kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha mfumo wa mafunzo ya kada za afya unaendana na mahitaji ya kisasa, maendeleo ya teknolojia, miongozo ya kitaaluma na mahitaji halisi ya soko la ajira.

Katika hatua hiyo, Serikali imeendelea kufanyia kazi maoni ya wadau na ushauri wa Kamati za Kudumu za Bunge kuhusu utekelezaji wa mitaala ya mafunzo katika baadhi ya fani za afya, ikiwemo Famasia, Uuguzi na Ukunga pamoja na Fiziotherapia.

Mhe. Mchengerwa amesema ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya Afya na Elimu ni muhimu katika kuhakikisha Taifa linapata wataalamu wa afya wenye ubora unaohitajika, sambamba na kujenga mfumo imara wa usimamizi na uendeshaji wa mafunzo ya kada hizo.

Aidha, Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuwashirikisha na kuwaelimisha wadau katika hatua mbalimbali za mabadiliko ya mitaala na vigezo vya udahili, ili kuhakikisha utekelezaji wa maboresho hayo unakuwa na uelewa wa pamoja na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wa usimamizi wa mafunzo, Serikali pia inaendelea kufanyia kazi ushauri wa kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya taasisi zinazohusika na elimu na mafunzo ya ufundi, pamoja na kutafuta mfumo bora zaidi wa kusimamia na kuendesha Vyuo vya Kati vya Afya.