BUHIGWE YAJIWEKA TAYARI KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MILIPUKO
Posted on: August 28th, 2026Na WAF - Kigoma
Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma imeendelea kuimarisha utayari wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko, ikiwemo ugonjwa wa Ebola, kwa kuhakikisha maeneo maalum ya kutolea huduma, vifaa tiba, dawa, magari ya dharura pamoja na mifumo ya utoaji wa huduma za dharura vinakuwa tayari muda wote, huku wananchi wakihimizwa kuendelea kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.
Hayo yamesemwa leo Agosti 27, 2026 mkoani Kigoma na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Wilaya ya Buhigwe Jenipha Msele, wakati wa ziara ya maafisa kutoka Wizara ya Afya Wilayani humo ambapo amesema Wilaya inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha maandalizi na kuhakikisha maeneo yote yanayohitaji maboresho yanafanyiwa kazi ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko na kuhakikisha usalama wa wananchi.
Amesema kuwa hadi sasa hakuna taarifa ya mtu anayeshukiwa kuwa na Ebola wala mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa huo katika Wilaya hiyo, lakini maandalizi yanaendelea ili kuhakikisha Wilaya inakuwa tayari kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe, Dkt. Baraka Kemero amesema maandalizi hayo yanawezesha hospitali kuwa katika nafasi nzuri ya kutoa huduma kwa wakati endapo kutatokea mgonjwa au mtu anayeshukiwa kuwa na ugonjwa wa mlipuko, huku akiwataka wananchi watakaohisi kuwa na dalili zinazoweza kuashiria ugonjwa huo kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi.
Aidha, Wizara ya Afya inaendelea na ziara na semina shirikishi katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha utayari wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko, ikiwemo kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa na watu wanaoshukiwa kuwa na Ebola yanakuwa tayari muda wote.
Hatua hizo zinafanyika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo CIHEB, kwa lengo la kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za dharura na uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko nchini, hususan katika mikoa ya Kigoma na Kagera ambayo inapakana na nchi zilizoathiriwa na ugonjwa huo.