Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WANANCHI MSIAMINI TAARIFA ZA UPOTOSHAJI - UMMY MWALIMU

Posted on: May 17th, 2022

Na. Catherine Sungura WAF-Dodoma


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka wananchi kutokuamini  taarifa za upotoshaji zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu chanjo nchini.


Waziri Ummy ameyasema hayo leo katika uzinduzi wa kampeni ya kutoa chanjo ya matone ya Polio kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.


"Hatutakubali kuona watu wachache kwa maslahi yao wakiiweka Tanzania  hatarini kwa ugonjwa wa Polio,Vyombo vya usalama wachukulieni  hatua wale wote wanaosambaza taarifa za uzushi na kupotosha jamii kuhusu chanjo,chanjo hizi ni salama"Alisema


Kwa upande wa chanjo Waziri huyo amesema kuwa lengo la kampeni hiyo ya utoaji wa chanjo ya matone ya Polio kwa watoto wote wenye umri wa miaka mitano  inayofanyika nchi nzima ni kuongeza kinga mwili kwa watoto na hivyo kuzuia kuenea kwa maambukizi ya Kirusi cha Polio kilichoripotiwa kuwepo ncho jirani ya Malawi.


Aidha, amesema kampeni hiyo itakua ni ya siku nne  na itafanyika  kwenye vituo vya huduma za afya pamoja na kuwafuata watoto mahali popote walipo.


Hata hivyo Waziri Ummy ameitaka Ofisi ya Rais-TAMISEMI kusimamia matumizi sahii ya fedha za chanjo zilizotolewa kwenye halmashauri zote nchini.


Jumla ya Watoto 10,295,316 wanatarajiwa kufikiwa  kwa Tanzania Bara na Zanzibar kwa awamu hii ya pili ambapo awamu ya kwanza iliyofanyika katika mikoa ya Njombe,Mbeya, Ruvuma na Songwe waliwafikia watoto 1,138,949 kati ya 983,542 waliokusudiwa.