Wizara Ya Afya

TANZANIA YAENDELEA KUIMARISHA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA EBOLA

Posted on: October 16th, 2026

Na WAF - Arusha

Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja sekta nyingine mtambuka imeanza kuweka mipango madhubuti ya kukabiliana na mlipuko wa Virusi vya Ebola ambao umeripotiwa nchi jirani ya Kenya baada ya kufanya ziara katika mpaka wa Namanga Mkoani Arusha.

Akiongelea ziara hiyo leo Oktoba 16, 2026, Mkoani Arusha, Mkurugenzi wa huduma za dharura na maafa kutoka Wizara ya Afya Dkt. Erasto Sylvanus amesema ziara hiyo maalum ya kutembelea mipaka ya karibu na nchi ya Kenya ina lengo la kuangalia utayari wa nchi kukabiliana na ugonjwa huo usiingie nchini na kuchukua hatua stahiki endapo kisa kitabainika.

"Lengo la ziara hii ni kuangalia maeneo ya kimkakati ili kuona namna nchi yetu ilivyojipanga kuzuia ugonjwa wa ebola usiingie nchini na endapo utaingia tuweze kukabiliana nao kwa njia sahihi na kuzuia kuenea kwa maambukizi", amesema Dkt. Erasto.

Ameongeza kuwa baada ya ugonjwa huo kuingia nchini Kenya, Tanzania imeimarisha afua mbalimbali ambazo zinasaidia kuhakikisha nchi inakua salama kwa kuweka mashine za kubaini joto kwa wasafiri katika mipaka wanapoingia nchini na endapo mhisiwa atabainika atawekwa sehemu maalum kwa ajili ya kufuatiliwa afya yake na kupewa huduma.

ameeleza kuwa, ziara hiyo ilianzia katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru ambako timu hiyo imeridhishwa na utayari wa Hospitali hiyo kwa wataalam kuwa na ufahamu wa ugonjwa huo, ameeleza elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi jinsi kujikinga, kuepuka kushika majimaji ya mtu, usafi wa mazingira pamoja na kutenga maeneo ya kunawa mikono.

Aidha, timu ya wataalam hao ilitembelea uwanja wa ndege wa Arusha na kuridhishwa na utayari uliowekwa kwa wasafiri kupimwa joto na kujaza taarifa zao kikamilifu ili iwe rahisi kufuatiliwa endapo maambukizi yatabainika au mhisiwa akipatikana.

Dkt. Erasto ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo na endapo kama mtu anahisiwa apige simu namba 199 kwa ajili ya kutoa taarifa na kuweza kufuatiliwa na kupewa huduma.