SERIKALI YAIMARISHA MAFUNZO YA WATAALAMU NA TEKNOLOJIA KATIKA HUDUMA ZA AFYA YA AKILI
Posted on: October 19th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF - Dodoma
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Bruno Sunguya amesema Serikali inaendelea kuimarisha mafunzo ya wataalamu na matumizi ya teknolojia katika huduma za afya ya akili nchini ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu mpya za mafunzo zinazolenga kupunguza upungufu wa wataalamu katika kada mbalimbali.
Prof. Sunguya amesema hayo leo Oktoba 19, 2026 wakati akitoa ufafanuzi wa hoja wakati wa majadiliano katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya Wizara ya Afya kuhusu hali ya afya ya akili, athari zake na mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.
"Hatua hii inatekelezwa kufuatia maelekezo ya Waziri wa Afya yaliyolenga kuimarisha mafunzo ya kitaalamu katika fani za tiba ya usemi, tiba ya viungo, saikolojia ya kitabibu na taaluma nyingine zinazochangia utoaji wa huduma bora za afya," amesema Prof. Sunguya
Ameeleza kuwa, baadhi ya programu hizo zimeanza kutoa wataalamu waliopata mafunzo ndani na nje ya nchi, hata hivyo, bado kuna uhitaji wa kuongeza idadi yao na kupanua wigo wa mafunzo ili huduma za afya ya akili ziweze kupatikana kwa urahisi hadi katika ngazi ya huduma za afya ya msingi.
Kuhusu matumizi ya teknolojia, Prof. Sunguya amesema, Serikali inaendelea kuangalia namna ya kutumia mifumo ya kidijitali, akili unde (AI) na teknolojia ya kujifunza kwa mashine (Machine Learning) katika kupanua upatikanaji wa huduma za afya ya akili na kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Aidha, Prof. Sunguya amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya taarifa na takwimu za afya ya akili pamoja na upatikanaji wa taarifa sahihi kutoka katika vyanzo vya kitaalamu, hatua itakayosaidia kukabiliana na taarifa zisizo sahihi zinazosambazwa kwa umma na kuboresha uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya afya ya akili.
Amesema, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau katika kuimarisha mafunzo, kuongeza wataalamu, kutumia teknolojia na kusogeza huduma karibu na wananchi, ili kuboresha utambuzi wa mapema na kuhakikisha watu wenye changamoto za afya ya akili wanapata huduma stahiki kwa wakati.