DKT SAMIZI ATOA WITO WA UCHUNGUZI WA MAPEMA SARATANI YA MATITI
Posted on: October 17th, 2026Na Shaban Juma, WAF – Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, ametoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kuchunguza afya zao na kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya wanapoona mabadiliko yasiyo ya kawaida katika matiti, ili kuongeza nafasi ya kupata matibabu kwa wakati.
Dkt. Samizi ametoa wito huo Oktoba 17, 2026, wakati akishiriki matembezi ya uhamasishaji wa Mwezi wa Saratani ya Matiti katika viwanja vya Taasisi ya Saratani Ocean Road, jijini Dar es Salaam, akimwakilisha Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Amesisitiza kuwa uhamasishaji wa saratani ya matiti ni muhimu katika kuongeza uelewa wa jamii, kuondoa hofu na dhana potofu kuhusu ugonjwa huo, pamoja na kuwahimiza wananchi kutafuta ushauri wa kitaalamu wanapobaini dalili zinazotia shaka.
Aidha, amewataka wananchi kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara, kula lishe bora, kudumisha uzito unaofaa kiafya, kuepuka matumizi ya tumbaku na kupunguza matumizi ya pombe, kama sehemu ya juhudi za kupunguza vihatarishi vinavyoweza kurekebishwa.
Dkt. Samizi ameeleza kuwa mapambano dhidi ya saratani ya matiti yanahitaji ushirikiano wa Serikali, wataalamu wa afya, wadau wa maendeleo, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha elimu sahihi inawafikia wananchi na wanaohitaji huduma wanafika katika vituo vya afya kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani, ikiwemo Taasisi ya Saratani Ocean Road, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma bora za Afya na za kisasa hapa nchini.
Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuendeleza ujumbe wa uhamasishaji huo katika familia, maeneo ya kazi na jamii zao, kwa kuzingatia kaulimbiu isemayo: “GUNDUA MAPEMA – CHUKUA HATUA MAPEMA – OKOA MAISHA.”