Wizara Ya Afya

SERIKALI YAIMARISHA KINGA YA MAGONJWA MIPAKANI KUPITIA UTAFITI WA NJIA ZISIZO RASMI

Posted on: September 15th, 2026

Na Andrea Kadege, WAF-Songwe

Serikali imeendelea kuimarisha kinga ya magonjwa katika maeneo ya mipakani kwa kutumia matokeo ya utafiti wa njia zisizo rasmi za kuvuka mipaka, unaolenga kubaini changamoto na maeneo hatarishi yanayoweza kuchangia kuenea kwa magonjwa ya mlipuko.

Akizungumza Septemba 15, 2026 wakati wa kufungua kikao cha kujadili matokeo ya mwaka mmoja wa utekelezaji wa afua hiyo mkoani Songwe, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt. Augustino Simon amesema taarifa zilizopatikana kupitia utafiti huo ni muhimu ili kuweka mikakati ya kuimarisha utayari, ufuatiliaji na mwitikio wa magonjwa kwa maeneo ya mipakani.

Amesema utekelezaji wa afua hiyo umeleta matokeo katika kuboresha mifumo na kujenga uwezo wa watumishi, pamoja na kuboresha baadhi ya miundombinu ya maeneo ya mpaka.

Kwa upande wake, Afisa Afya kutoka Wizara ya Afya, Bw. Athanas Lucas, amesema ni muhimu taarifa zilizokusanywa katika Wilaya za Momba na Ileje zitumike kwa ajili ya kupanga hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto zilizobainika katika njia hizo zisizo rasmi.

Amesema utafiti huo umewezesha kutambua maeneo na changamoto zinazohitaji hatua za haraka, huku akisisitiza umuhimu wa Serikali na wadau kutumia taarifa hizo kuimarisha uwezo wa kutambua na kudhibiti magonjwa kabla hayajasambaa.

Ameongeza kuwa maandalizi yaliyofanyika kukabiliana na magonjwa kama Mpox yanaweza kutumika pia katika kuimarisha utayari dhidi ya magonjwa mengine ya mlipuko, ikiwemo Ebola, kutokana na uwepo wa mwingiliano wa watu katika maeneo ya mipakani.

Kwa upande wake Mkuu wa Kliniki na Mtaalamu wa Masuala ya Afya na Uhamaji wa IOM, Dkt. Thomas Kalasani amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, Wizara ya Afya na wadau kwa kutekeleza hatua zitakazotokana na utafiti huo, akieleza kuwa taarifa hizo zinapaswa kugeuzwa kuwa hatua zinazolenga kuziba mapungufu yaliyobainika na kuimarisha ulinzi wa afya kwa wananchi wanaoishi na kufanya shughuli zao katika maeneo ya mipakani.