Wizara Ya Afya

MIONGOZO YA KITAALAMU KUIMARISHA UBORA WA HUDUMA ZA MAABARA NCHINI

Posted on: August 28th, 2026

Na Cletus Sanga, WAF – Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu na CIHEB Tanzania chini ya Usalama wa Afya Duniani imeendelea kuimarisha huduma za maabara nchini kupitia usambazaji wa miongozo ya kitaalamu inayolenga kuboresha ubora, usalama na ufanisi wa huduma za uchunguzi wa magonjwa.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 28 Agosti na kaimu Mganga Mkuu wa Serikali wakati wa kikao kazi cha usambazaji wa miongozo ya kuboresha huduma za maabara, Jijini Dodoma.

Dkt. Eliakim amesema miongozo hiyo ni nyenzo muhimu katika kuwawezesha wataalamu kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viwango na taratibu za kitaalamu.

“Ni muhimu kuhakikisha miongozo inawafikia watendaji na inatumika ipasavyo katika maeneo ya huduma, kwa kuwa huduma bora za maabara zina mchango mkubwa katika kupata majibu sahihi ya uchunguzi na kusaidia wataalamu kufanya maamuzi sahihi ya kitabibu,” amesema Dkt. Eliakim.

Amesema matumizi sahihi ya miongozo hiyo yataongeza uelewa wa watendaji kuhusu taratibu za utoaji wa huduma, huku yakisaidia kuimarisha usalama wa wafanyakazi wa maabara na kuongeza ufanisi katika huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Huduma za Maabara kutoka Wizara ya Afya, Bw. Reuben Mkala amesema usambazaji wa miongozo hiyo utasaidia kuwafikia watendaji katika ngazi mbalimbali na kuwawezesha kutumia nyaraka hizo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Naye, Mwakilishi kutoka CIHEB Tanzania Bw. Jacob Lusekelo amesema hatua ya kusambaza nyaraka hizo ni muhimu katika kuhakikisha watendaji wanakuwa na rejea zinazowaongoza katika utekelezaji wa majukumu yao, hasa katika huduma za uchunguzi zinazohitaji usahihi, usalama na ufuataji wa viwango vya kitaalamu.

Amesema miongoni mwa nyaraka zinazowasilishwa ni Orodha ya Taifa ya Uchunguzi Muhimu wa Magonjwa, pamoja na miongozo ya ulinzi na usalama wa wafanyakazi wa maabara na nyaraka nyingine zinazolenga kuimarisha mifumo ya huduma za maabara nchini.