Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MIFUMO YA SEKTA YA AFYA KUIMARISHWA ZAIDI.

Posted on: March 8th, 2024



Na. WAF – Dar Es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya afya imedhamiria kuendelea kuimarisha mifumo ya Sekta ya Afya itakayomuwezesha mwananchi kupata huduma bora za Afya popote nchini bila kikwazo chochote.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu Marchi 7, 2024 Jijini Dar Es Salaam katika kikao kazi cha wadau kutoka Serikali ya Ujerumani na Uingereza cha kufanya tathimini ya Mradi wa Backup Health ulioanza mwaka 2020 na kutarajiwa kumalizika Machi 30, 2024 ambao uligharimu kiasi cha Euro milioni tatu ukiwa na lengo la kuimarisha mifumo ya Afya nchini huku ukifanyika maeneo ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Dkt. Jingu amesema kupitia mradi huu mifumo mingi imeweza kuimarika ikiwemo mifumo ya kidigitali itamuwezesha mwananchi kupata huduma za afya zilizo bora wanazostahili bila kikwazo chochote hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika mfumo wa bima ya Afya kwa wote.

“Ugharamiaji wa sekta ya Afya ni jambo kubwa, unaweza kuwa na pesa leo lakini kesho usiwenayo na magonjwa huwa hayapigi hodi, lakini tukiwa na mifumo imara itawawezesha watanzani kupata huduma za afya hata kwa wale ambao hawatakuwa na pesa hili ni jambo tulilodhamiria kama nchi kupitia amaelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya utekelezaji wa sheria ya Bima ya afya na mifumo mingineyo tuliyoiweka ambayo itasaidia mtanzania yeyote kupata huduma za afya kokote alipo bila kikwazo chochote na mradi huu umechangia katika kusaidia kuimarisha jitihada hizo” amesema Dkt. Jingu.

Dkt. Jingu amewapongeza na kuwashukuru wadau hao kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha sekta ya afya Tanzania na kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora za afya na kuendelea kushirikiana na serikali hata baada ya mradi huu kuisha.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Programu kutoka (German Cooperation-GIZ)-BACKUP Health, Bw. Huzeifa Bodal amebainisha kuwa Ujerumani imekuwa na mchango katika kuboresha mifumo ya afya hii ni katika mashirikiano ya Kimataifa baina ya nchi hizo mbili aidha programu hiyo imesaidia kuboresha ufanisi wa huduma za afya, kushirikiana na jamii na kuongeza ushirikiano kati ya Serikali na vituo vya afya nchini.