Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

KONGAMANO LA KWANZA LA KISAYANSI KUHUSU TIBA ASILI LAFANYIKA MKOANI MOROGORO

Posted on: August 29th, 2022


Na. Catherine Sungura, Morogoro


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itakua bega kwa bega  na waganga wa Tiba Asili katika kuhakikisha tafiti na mafunzo ya kazi zao yanakuwa endelevu na za zenye ubora unaotakiwa.


Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Uzamili na utafiti kutoka SUA Prof.  Esron Karimuribo wakati wa Kongamano la kwanza la Kisayansi la kuhusu Tiba asili ya Mwafrika linalofanyika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Mkoani Morogoro.


Prof. Karimuribo amesema kuwa Chuo cha SUA  kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na wadau mbalimbali wameandaa kongamano hilo lenye lengo la kuibua ubunifu  na kupata suluhisho la kisayansi kuhusu changamoto zilizoko kwenye mnyororo wa thamani wa biashara ya bidhaa za mimea dawa hapa nchini.


“Kwenye biashara ya bidhaa za mimea dawa ni muhimu sana katika kukuza na kuendeleza biashara za aina hii, hii ni kwa sababau pamoja na kuwepo matumizi ya dawa hizi kuwepo kwa biashara hii karne kwa karne, bado uibuaji wa ubunifu umekuwa mdogo na umekuwa ukifanywa na mdau mmoja mmoja”.


Hata hivyo amesema bado kuna changamoto  mbalimbali zikiwemo za uzalishaji hasa wa mali ghafi za uanzishaji na uendelezaji wa viwanda hasa wa mali ghafi hizo,masuala ya masoko na za kisera.


Ameongeza kuwa kongamano hili litasaidia kuibua ubunifu na kuendeleza na kujaribu kupunguza changamoto za uzalishaji na za kibiashara zilizopo au zinazoweza kujitokeza katika biashara nziama za bidhaa za tiba asili.


Naye Mkurugenzi wa Idara ya tiba kutoka Wizara ya afya aliyeshiriki kongamano hilo kwa nia ya mtandao Dkt. Omary Ubuguyu amewataka watafiti kusaidiana katika utekelezaji wa tafiti ili kuwa na matokeo chanya yatakayo kuwa na ufuatiliaji kwenye eneo la tiba asili pamoja na kufuatilia athari zinazotokana na matumizi ya dawa.


Amesema kuwa Wizara ya Afya imeweza kuandaa muongozo wa matibabu ya tiba asili kwenye hospitali pia muongozo wa mafunzo wa Tiba asili.


“Mnyororo wa utoaji wa huduma katika huduma za tiba asili kwenye hospitali itatupa huduma nzuri na sasa tumeanza kupitia baadhi ya dawa na malengo yetu ni kutumia hospitali zetu za rufaa za Mikoa.

Dkt. Ubuguyu amewataka washiriki hao kuwa na ushirikiano wa pamoja ili kuwa na matokeo yanayowalenga Watanzania hivyo kuwa tayari katika ushirikiano katika tiba asili.


Kongamano hilo linawahusisha pia Umoja wa watengeneza dawa Tanzania(UWABIATA), Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali na wadau wengine ambapo mijadala na mawasilisho katika kongamano hilo litajikita katika utafiti na maendeleo ya tiba asili, Tiba asili na magonjwa yasiyoambukiza, tiba asili na maendeleo ya viwanda, tiba asili na uthibiti na masoko ya bidhaa ya tiba asili pamoja na kilimo cha mimea dawa.


-Mwisho-