Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

BARAZA LA TIBA ASILI LAELEKEZWA KUIMARISHA USIMAMIAJI WA SHERIA ILI KUONDOA DAWA ZA ASILI ZISIZOFAA KATIKA JAMII.

Posted on: September 14th, 2023

Na WAF- DSM


MWENYEKITI wa kamati ya Bunge ya kudumu ya Afya na masuala ya UKIMWI Mhe. Stanslaus Nyongo amelitaka Baraza la Tiba asili na Tiba mbadala kuimarisha usimamiaji wa Sheria ili kuondoa changamoto ya uwepo wa dawa za asili zisizofaa katika jamii. 


Mhe. Nyongo amesema hayo alipoungana na wajumbe wengine wa kamati ya kudumu ya Bunge ya afya na masuala ya UKIMWI kutembelea katika Taasisi ya NIMR kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa katika taasisi hiyo hasa katika eneo la tafiti za tiba asili. 


"Baraza lifanye kazi yake ili kuondoa Waganga wababaishaji wa tiba asili wote, wanaouza dawa za asili na kusema kwamba, dawa hizi zinatibu magonjwa mbalimbali, inatibu kisukari, inaitibu UKIMWI, inatibu COVID, inatibu nguvu za kiume n.k". Amesema Mhe. Nyongo. 


Mhe. Nyongo ameendelea kusisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara kuweka mkazo katika Sheria ya tiba asili, ili kuhakikisha mtu yoyote anaeuza dawa mahali popote katika soko la dawa auze dawa ambazo ni salama kwa mtumiaji ambaye ndio Mtanzania.


Aidha, Mhe. Nyongo amewataka Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) kuimarisha zaidi kwenye kufanya tafiti za tiba asili na tiba mbadala ili kuhakikisha dawa zinazoingia katika soko la wananchi hazileti madhara kwa wananchi lakini zinaongeza ufanisi wa nguvu ya kutibu.


Nae, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt. Faustine Ndugulile ameutaka uongozi wa NIMR kuhakikisha wanatafuta kiasi cha shilingi milioni 160 ili kumaliza uwekezaji wa mashine ya kutengeneza dawa ambayo mpaka sasa imegharimu zaidi ya Bilioni 2 na wananchi waanze kunufaika na uwekezaji huo. 


Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya ipitie upya Sheria za kudhibiti matangazo horera kuhusu dawa za tiba asili na tiba mbadala kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari ambayo yamekuwa takipotosha jamii kuhusu dawa hizo, huku nyingi kati ya dawa hizo zikikikosa kigezo cha usalama.