Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

BADILISHENI MTINDO WA MAISHA - PROF. JANABI

Posted on: February 15th, 2024



Wananchi wameaswa kubadilisha mtindo wa maisha ili kuwa na afya njema na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Prof. Mohamed Janabi katika hafla ya ugawaji tuzo za HUMANITARIAN AWARD ambazo zimelenga kutambua mchango wa ubinadamu unaofanywa na wadau mbalimbali zilizoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Professor Jay Foundation Jijini Dar es salaam katika Ukumbi wa Ummy Mwalimu uliopo Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Prof. Janabi amewataka wananchi kubadili mtindo wa maisha ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza kama Kisukari, Shinikizo la Damu, Kiharusi, Ugonjwa wa Figo.

"Kinga ni Bora kuliko tiba ni vyema kupunguza matumizi ya sukari pia haina haja ya kwenda 'gym' unaweza kutembea angalau hatua 10 kwa siku, hakuna chakula tunasema usile, kula kwa kiasi ila kula vyakula vyenye Afya, punguza kula vyakula vya kusindika". Amesema Prof. Janabi

Nae mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Bi. Grace Msemwa amesema Wizara ina jukumu la kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya masuala mbalimbali ya afya ikiwemo mabadiliko chanya ya tabia na kufanya uchunguzi wa awali wa afya.

"Jamii iendelee kufuatilia taarifa sahihi za namna ya kujikinga na Magonjwa yasiyoambukiza na yanayoambukiza, ili kupata taarifa hizo kwa usahihi wananchi wanashauriwa kupiga simu namba 199 bure. Amesema. Bi Grace.

Aidha, Bi Grace amepokea tuzo iliyotolewa kwa Wizara ya Afya kutokana na mchango mkubwa katika utoaji wa Elimu kwa jamii kuhusu Afya.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo @professorjayfoundation Bw. Florian Rutabingwa ameelezea ujio wa program maalumu inayoandaliwa kwa ushirikiano mkubwa na wizara ya afya kupitia Sehemu ya Elimu ya Afya kwa umma, 'AFYA NA MUZIKI TOUR' ambayo inalenga kuzunguka nchi nzima kutoa elimu ya afya kwa wananchi kuhusu magonjwa yakuambukizwa na yasiyoambukizwa lakini pia kuwezesha upimaji wa afya kwa wananchi hususani kwenye magonjwa yasiyo ya kuambukizwa.