Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WATANZANIA WATAKIWA KUONDOA UNYANYAPAA UNAOHUSIANA NA HEDHI KWA WASICHANA, WANAWAKE

Posted on: May 27th, 2025

Na WAF - Dodoma


Watanzania wametakiwa kuachana na tabia za unyanyapaa, mila potofu na kuweka mazingira wezeshi kwa wasichana na wanawake wakati wa hedhi kwa kuwa hedhi si laana, si uchafu wala jambo la kuogopwa bali ni alama ya afya, uzazi, na mwanzo wa utu wa msichana.


Kaimu Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya Dkt. Otilia Gowele akimuwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Jensita Mhagama amesema hayo leo Mei 28, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Wizara ya Afya Dodoma ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Hedhi Salama ambayo huadhimishwa  ifikapo Mei 28 kila mwaka.


"Lakini pia niwaombe wazazi, tuwape watoto wetu elimu sahihi na ya upendo kuhusu miili yao na kuwanunulia bidhaa salama za hedhi, vilevile walimu, tuwasaidie wanafunzi kuelewa mabadiliko ya miili yao bila kuwaaibisha, namna ya kujisitiri na utupaji sahihi wa bidhaa za hedhi zilizotumika," amesema Dkt. Gowele.


Aidha, Dkt. Gowele amesema taarifa ya hali ya uchumi iliyotolewa na Benki ya Dunia mwaka 2023 inaonesha wanafunzi wa kike waliopevuka hupoteza wastani wa siku 30-40 za masomo kila mwaka kutokana na kukosekana kwa mazingira wezeshi shuleni wakiwa kwenye hedhi.


Pia amesema, taarifa ya Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR 2021) imebainisha wasichana takribani asilimia 17 walishindwa kuhudhuria masomo yao pindi wakiwa katika hedhi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo  maumivu ya tumbo 74%, kuogopa fedheha endapo wangechafuka 34%, na kukosa vifaa salama vya hedhi 42%.


"Wizara inatekeleza kampeni ya Mtu Ni Afya awamu ya Pili ambayo ilizunduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango Mei 9, 2024, inayohamasisha na kuhimiza tabia zinazoondosha unyanyapaa, mila potofu kwa wasichana na wanawake wakati wa hedhi," amesema Dkt. Gowele


Amesema. Serikali itaendelea kuweka mazingira salama na miongozo inayoendana na afua zote za hedhi salama katika kuhakikisha suala la hedhi salama linapewa uzito na kushirikisha jamii kwa upana wake, inaendelea kutatua changamoto za hedhi salama ikiwemo upatikanaji wa pedi kwa wasichana wa rika balehe walioko kwenye shule za msingi na sekondari.


Maadhimisho ya Siku ya Hedhi Salama mwaka huu Kitaifa yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Wezesha Mazingira ya Hedhi Salama yenye Utu kwa Wasichana na Wanawake Wote,' ambapo uwezeshaji utawezesha kuleta maendeleo na utu kwa msichana na mwanamke.