Customer Feedback Centre

Ministry of Health

UWEKEZAJI ULIYOFANYIKA UENDANE NA UBORA WA HUDUMA HOSPITALI YA KANDA KUSINI- MTWARA

Posted on: September 15th, 2023

Na. WAF, Mtwara.


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka watumishi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini kuhakikisha kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Samia Suluh Hassan katika Hospitali hiyo ikiwemo ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa, kuajiri watumishi pamoja na uhakika wa upatikanaji wa dawa unaendana na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.


Waziri Ummy ametoa wito huo leo Septemba 15,2023 wakati akizungumza na Watumishi wa Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua Hospitali hiyo


Aidha Mhe. Ummy amewapongeza watumishi kwa huduma bora zinazotolewa huku akiwasitiza kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, maadili na viapo vya Taaluma zao.


“Niwapongeze sana kwa huduma bora mnazozitoa, hospitali hii ina jengo zuri sana, vifaa tiba kwaiyo kilichobaki ni ubora wa huduma”. Ameeleza Waziri Ummy 


Mhe. Ummy Mwalimu amewahakikishia watumishi wa hospitali hiyo kuwapatia gari aina ya Coaster moja kwa ajili ya kuwarahisishia kufika kazini.


“Tutaleta angalau gari moja ili kuwarahisishia watumishi kufika kwa wakati eneo la kutolea huduma” , amesisitiza Waziri Ummy.


Waziri Ummy amesema kuwa ataendelea kuwa balozi wao kwa kuwasema, kuwalinda, pamoja na kuwatekelezea stahiki zao lakini kila mtumishi atimize wajibu wake ili kuleta ubora wa Huduma kwa wananchi wanao wahudumia.