Ministry of Health

SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA URATIBU WA MAPAMBANO DHIDI YA USUGUVU WA VIMELEA DHIDI YA DAWA

Posted on: October 1st, 2026

Na Andrea Kadege, WAF–Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Amref Health Africa-Tanzania chini ya ufadhili wa UK International Development na sekta mbalimbali zinazounda Afya Moja, imeendelea kuimarisha uratibu wa mapambano dhidi ya Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa (UVIDA) kupitia Kikao cha 33 cha Kitaifa cha Sekta Mbalimbali zinazounda Afya Moja kuhusu UVIDA.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika leo Oktoba 01, 2026 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Uratibu ya UVIDA, Prof. Hezron Nonga, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na UVIDA, huku akihimiza wajumbe kuongeza ushirikiano na kasi ya utekelezaji wa shughuli za kukabiliana na changamoto hiyo kupitia dhana ya Afya Moja.

"UVIDA ni changamoto inayoweza kupunguza ufanisi wa dawa zinazotumika kutibu maambukizi, hivyo kuathiri usalama wa wagonjwa na kuongeza gharama na muda wa matibabu, hali hiyo pia inaweza kuongeza hatari ya maambukizi kuwa magumu zaidi kutibiwa" amesema Prof. Nonga

Aidha amesema dhana hiyo inahitaji ushirikiano wa karibu kati ya sekta za afya, mifugo, kilimo na mazingira, kwa kuwa usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni changamoto inayogusa maeneo yote na haiwezi kudhibitiwa na sekta moja pekee.

Kwa kuzingatia hilo, kikao hicho kinatoa fursa kwa sekta mbalimbali kupitia utekelezaji wa afua, kubadilishana taarifa na kuimarisha hatua za pamoja katika maeneo ya kinga, matumizi sahihi ya dawa, ufuatiliaji wa usugu na udhibiti wa maambukizi.

Amesisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa na mwelekeo mmoja katika kukabiliana na UVIDA, kulinda ufanisi wa dawa zilizopo na kuhakikisha zinabaki kuwa na manufaa kwa afya ya binadamu, wanyama na jamii kwa ujumla.