Ministry of Health

RUFIJI YAPATA HUDUMA ZA AFYA KARIBU, SAFARI ZA LINDI NA TUMBI KUPUNGUA

Posted on: October 4th, 2026

Na WAF – RUFIJI

Naibu Waziri wa Afya, Mhe.Dkt. Florence Samizi amesema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika huduma za afya Wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani umewezesha wananchi kupata huduma karibu na maeneo yao, hatua itakayopunguza safari za kwenda Lindi na Hospitali ya Tumbi kutafuta huduma za matibabu.

Mhe. Samizi amesema hayo Oktoba 4, 2026 wakati wa akishiriki zoezi la hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na Ujenzi wa chuo cha Afya Samia Suluhu Hassan Wilayani Rufiji, ambapo ameeleza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za afya kwa urahisi na kwa wakati.

Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipohutubia Bunge mwezi Novemba 2025 alisisitiza umuhimu wa huduma kumfikia mwananchi badala ya mwananchi kulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo.

“Mheshimiwa Rais alipohutubia Bunge mwezi wa 11 mwaka 2025 alisema anataka huduma zimfuate mwananchi na si mwananchi afuate huduma. Lakini alisema anataka kumwachia Mtanzania tabasamu. Leo hii Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha kwa vitendo kwamba wananchi wa Rufiji sasa hawatakwenda Lindi, wananchi wa Rufiji sasa hawatakwenda Tumbi. Huduma zimewafuata hapa,” amesema Mhe.Dkt. Samizi.

Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini, hususan huduma za mama na mtoto, ambazo ni miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele katika juhudi za kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.

Kwa mujibu wa Mhe. Samizi, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha huduma za afya na kupunguza vifo vya mama na mtoto, akieleza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika eneo hilo.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye kinara wa kupunguza vifo vya mama na mtoto Afrika, si Tanzania, Afrika, nchi zaidi ya 54. Amepewa ukinara huo si kwa sifa, lakini ni kwa mambo makubwa mazito aliyoyafanya kwenye nchi yetu kwa sababu amepunguza vifo vya mama na mtoto kwa asilimia 80,” amesema.