Customer Feedback Centre

Ministry of Health

DOZI MOJA YA CHANJO YA HPV INATOSHA KUMKINGA MSICHANA KUPATA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI

Posted on: April 22nd, 2024



Na WAF - Mwanza

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema dozi Moja ya chanjo ya HPV inatosha kumkinga msichana kupata ugonjwa wa Saratani ya Mlango wa Kizazi na kuwataka wazazi/walezi kuwapeleka watoto kupata chanjo hiyo.

Waziri Ummy Mwalimu amesema hayo leo Aprili 22, 2024 kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya Dozi moja ya chanjo ya HPV kwa wasichana wenye umri wa miaka 9 hadi 14 iliyozinguliwa katika viwanja vya Furahisha Wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza.

“Wataalamu wetu ambao wanatoka kwenye Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) wametuhakikishia kuwa dozi moja ya chanjo ya HPV inatosha kumkinga msichana kupata Saratani ya Mlango wa Kizazi”. Amesema Waziri Ummy

Amesema, awali dozi zilizokuwa zinatolewa mbili, ya kwanza inatolewa leo na baada ya miezi Sita inatolewa nyingine hii ilikua inapelekea mabinti wengi kutorudi kupata dozi ya pili, Sasa hivi tumeamua kutoa dozi moja ya HPV kwa kuwa inatosha kuwakinga wasichana kuja kupata maambukizi ya Saratani ya Mlango wa Kizazi.

Aidha, Waziri Ummy amesema Saratani inayoongoza kuwatesa Watanzania ni Saratani ya Mlango wa Kizazi ambapo amesema katika kila wagonjwa 100 wanaougua Saratani, wagonjwa 23 ni wagonjwa wa Saratani ya Mlango wa Kizazi.

“Inafuata Saratani ya mfumo wa chakula asilimia 11, Saratani ya Matiti asilimia 10.4, Saratani ya tezi dume asilimia 8.9 kwa hiyo ukiaangalia hapo Saratani inayoongoza ni Saratani ya Mlango wa Kizazi”. Amesema Waziri Ummy

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe. Saidi Mtanda amesema watahakikisha watoto wote wenye umri wa kuanzia miaka 9-14 wanapata chanjo hiyo ili kufikia malengo.

“Kwa mwaka 2022/23 Mkoa wa Mwanza ulifanikiwa kuchanja watoto zaidi ya laki Mbili sawa na asilimia 107 kati ya walengwa waliotarajiwa kuchanjwa ni laki 191,440 wenye umri chini ya Mwaka Mmoja, tumefikia malengo na kuyavuka”. Amesema Mhe. Makilagi