Customer Feedback Centre

Ministry of Health

BIMA YA AFYA KWA WOTE WATOKA NA MAAZIMIO SABA MUHIMU

Posted on: November 1st, 2024

Na WAF – Arusha.
 
Kongamano la Bima ya Afya kwa Wote na Jukwaa la Ugharamiaji wa huduma za afya limehitimishwa leo huku wataalamu na wadau wa sekta ya afya wakikubaliana kutekeleza maazimio saba (7) yatakayosaidia utekelezaji wa ufanisi wa huduma za Bima ya Afya kwa Wote.
 
Akifunga kongamano hilo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Novemba Mosi, 2024, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Afya Bw. Issa Ng’imba amesema Wataalamu pamoja na wadau wa sekta ya afya wametumia siku nne za mafanikio kupanga na kuazimia utekelezaji wa maazimio saba.
 
“Katika siku nne tulizokaa hapa kama Wataalamu waliobobea katika sekta ya afya, kwa pamoja tumetoka na mikakati na mipango itakayotupeleka mbele ili kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote na kuwa na vyanzo endelevu vya kugharamia huduma za afya nchini Tanzania,” amesema Bw. Ng’imba.
 
Amesema azimio la kwanza ni wataalamu wa sekta kukubaliana  kutumia utaalamu wao kupata au kuongeza rasilimali fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa bima ya afya kwa wote. 
 
Azimio la pili amesema kuwa ni kuandaa mkakati wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ambao utabainisha majukumu na wajibu wa wadau wote wa sekta ya afya na hapa amesisitiza kuwa suala la bima ya afya kwa wote siyo jukumu la sekta ya afya pekee.
 
"Wataalamu wamekubaliana pia kuhakikisha viwango vya uchangiaji kwa wanachama vinazingatia uwezo na kuwa na namna bora ya uchangiaji hususan kwa sekta isiyo rasmi," amesema Bw. Ng’imba
 
Azimio la nne, amesema kuwa ni kuandaa mpango mkakati wa kutekeleza dhana ya ulazima kwa watu wote kujiunga na bima.

Aidha ameeleza azimio lingine kuwa ni kuandaa mpango shirikishi wa utoaji wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya kwa kuwashirikisha wadau wote.
 
Amesema pia azimio la saba ni Serikali kuendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali katika dhana nzima ya utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.