Ministry of Health

AGA KHAN YAWEKEZA SHILINGI BILIONI 1.3 KUIMARISHA HUDUMA ZA KINYWA NA MENO

Posted on: October 3rd, 2026

Na Andrea Kadege, WAF–Dar es Salaam

Hospitali ya Aga Khan Health Service Tanzania imewekeza takribani Shilingi bilioni 1.3 katika kuanzisha Kituo cha Huduma za Meno na Vipandikizi katika Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam, ikiwa ni hatua ya kuongeza uwezo wa kutoa huduma maalumu na za kisasa za afya ya kinywa nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kituo hicho Oktoba 2, 2026, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Daud Tayari amesema uwekezaji huo unaonesha mchango wa sekta binafsi na taasisi zisizo za kiserikali katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha mfumo wa afya.

“Uwekezaji huu unaonesha pia nafasi muhimu ya sekta binafsi na sekta isiyo ya kiserikali katika kukamilisha juhudi za Serikali za kuimarisha mfumo wa afya nchini,” amesema Bw. Tayari

Amesema kuwa kituo hicho kina vyumba sita vya kisasa vilivyo na vifaa kamili na kinatoa huduma mbalimbali zikiwemo huduma za jumla za meno, urejeshaji wa meno yaliyoharibika, upangaji wa meno na vipandikizi vya meno.

Bw. Tayari amesema Hospitali ya Aga Khan imeendelea kuchangia maendeleo ya huduma za afya nchini kupitia uwekezaji katika miundombinu, teknolojia, rasilimali watu na maboresho ya ubora wa huduma.

Aidha ametumia fursa hiyo kuwataka kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote ambayo mpango wake unakwenda kutekelezwa hivi karibuni kwa awamu ya pili, ikiwemo utoaji wa huduma za kinywa na meno kwa wananchi.

Amesisitiza kuwa pamoja na uwekezaji katika teknolojia na miundombinu, kinga inapaswa kupewa kipaumbele, akiwataka wananchi kufanya uchunguzi wa meno mara kwa mara na kutafuta matibabu mapema ili kusaidia kuhifadhi meno yao ya asili kwa muda mrefu.