WIZARA YA AFYA YATOA MSUKUMO MPYA KWA WATUMISHI KUSIMAMIA AFYA MIPAKANI
Posted on: September 17th, 2026Na Andrea Kadege, WAF-Songwe
Wizara ya Afya kupitia Idara ya Kinga, Sehemu ya Afya Mipakani, kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), imeendelea kuimarisha uwezo kwa watumishi wa afya Mkoani Songwe ili kusimamia masuala ya afya katika maeneo ya mipaka.
Zoezi hilo limefanyika leo, Septemba 17, 2026, katika eneo la mpaka kati ya Tanzania na Zambia (Tunduma) kupitia zoezi la usimamizi shirikishi na kuwajengea uwezo watumishi wa afya, sambamba na kufanya tathmini ya matokeo ya zoezi la utambuzi wa njia zisizo rasmi lililofanyika katika maeneo ya Mkoa wa Songwe.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Afya kutoka Wizara ya Afya, Josephine Kapinga amesema uimarishaji wa uwezo wa watumishi wa afya ni sehemu muhimu ya kuhakikisha shughuli za afya mipakani zinatekelezwa kwa ufanisi, hususan katika maeneo yenye mwingiliano mkubwa wa watu kutoka Tanzania na nchi jirani.
Amesema uwepo wa taarifa sahihi kuhusu maeneo na mienendo ya watu wanaotumia njia zisizo rasmi unaweza kusaidia mamlaka za afya kuelewa mazingira ya maeneo hayo na kupanga afua zinazolingana na mahitaji ya jamii.
Katika zoezi hilo, watumishi wa afya wamepata fursa ya kupitia matokeo ya utambuzi wa njia zisizo rasmi na kujadili namna taarifa hizo zinavyoweza kutumika katika kuboresha ufuatiliaji wa afya, mawasiliano ya taarifa na utekelezaji wa hatua za kinga katika maeneo yanayozunguka mipaka.
Aidha, ameeleza kuwa usimamizi huo pia unalenga kusaidia kuongeza matumizi ya taarifa katika kupanga afua na kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na vihatarishi vya afya vinavyoweza kujitokeza katika jamii za mipakani.
Jitihada hizo zinaunga mkono azma ya kuimarisha kinga, ufuatiliaji na mwitikio wa afya katika maeneo ya mipakani, huku zikilenga kuhakikisha jamii zinazoishi na kusafiri katika maeneo hayo zinapata ulinzi bora dhidi ya vihatarishi vya afya.